TAARIFA YA JESHI LA ZIMA MOTO NA UOKOAJI MWAKA 2020

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa taarifa kwa umma, kuanzia mwezi Januari, 2020 hadi Disemba, 2020 limekabiliana na matukio mbalimbali ya moto, maokozi na ajali za barabarani. Pamoja na kukabiliana na matukio hayo pia limeendelea kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto, kutoa elimu kwa umma Pamoja na kufanya uchunguzi wa matukio ya moto.


Katika kipindi cha Januari hadi Disemba, 2020 Jeshi limekabiliana na matukio ya moto

1925 ambayo yamesababisha vifo vya watu 62, kati ya hao Wanaume 45, Wanawake 17, pia matukio hayo yalisababisha majeruhi 74 kati ya hao Wanaume 52 na Wanawake 22.

Pia Jeshi limefanya maokozi katika maeneo mbalimbali zikiwemo ajali za barabarani, mafuriko, kwenye migodi, mashimo ya vyoo, mito, mabwawa, baharini pamoja na maeneo mengine. Jumla ya maokozi 845 yalifanyika, matukio hayo ya maokozi yalisababisha vifo 495 kati ya hao Wanaume ni 402 na Wanawake 93. Pia maokozi hayo yalikuwa na majeruhi 817 kati ya hao Wanaume ni 570 na Wanawake 247.

Aidha katika kutafuta sababu za matukio hayo. Jeshi linautaratibu wa kufanya uchunguzi ili kubaini vyanzo na kutoa taarifa kwa umma pamoja na ushauri ili kupunguza matukio hayo kujirudia.

Baada ya kufanya uchunguzi, baadhi ya maeneo tumetoa maelekezo na kushauri ili kupata muarobaini wa tatizo. Kama mnavyojua hivi karibuni tumekuwa na matukio mengi ya kuungua kwa shule. Shule zipatazo 44 zimeungua na kusababisha   kupoteza Maisha kwa  baadhi ya wanafunzi, kuharibu miundombinu na kuteketea kwa vifaa vingi .

 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limebaini majanga mengi ya moto yanatokana na uzembe, hujuma na hitilafu za umeme. Hata hivyo kwa upande wa shule za bweni tumebaini Wanafunzi wanachaji simu kwa kificho kwa kutumia nyaya za umeme zilizopita darini, kutumia heater, kutumia pasi bila kuwa waangalifu, mishumaa wakati umeme ukikatika, pamoja na kutumia taa zinazotumia mafuta sehemu ambazo hakuna umeme.

Ili kupunguza    majanga ya moto shuleni, Jeshi limeingia makubaliano na Chama cha Skauti Tanzania, kutoa elimu kwa wanafunzi baada ya wao kupatiwa mafunzo ya utoaji elimu ya kinga na tahadhari ya majanga ya moto, Skauti watakuwa sehemu ya wazimamoto wa kujitolea. Pia Jeshi limeweza kuanzisha klabu rafiki za Zimamoto katika shule za Msingi na Sekondari, tuna jumla ya klabu 786 zenye wanachama 34,018.

Aidha Jeshi lina mikakati ya kuongeza vitendea kazi katika Mikoa na Wilaya, kama mnavyojua hivi karibuni tumeingia makubaliano na Shirika la Nyumbu, kutengeneza magari mabovu na kununua magari mapya kupitia shirika hilo.

Kuongeza utoaji elimu kwa umma kwa kutumia vyombo vya habari, tunategemea kutumia vyombo vya habari kutoa elimu kwa umma kwa kufanya vipindi vingi vya kuelimisha ili kuyafikia maeneo mengi zaidi.

Kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto kwenye maeneo yote ya mikusanyiko ya watu zikiwemo shule zote za bweni na za kutwa ambazo hivi karibuni zimeshambuliwa na majanga ya moto.

Kwa huduma ya haraka juu ya majanga ya moto na maokozi Piga namba 114.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post