RC TELACK ATOA MSAADA WA CHAKULA KWA VITUO VYA KULELEA WATOTO YATIMA SHINYANGA

Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akimkabidhi mchele Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kituo cha kulelea watoto yatima Mjini Shinyanga 'Shinyanga Society Orphans', Bi. Ayam Ally Said. 

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ametoa msaada wa magunia 17 (tani 1.7) ya mchele yenye thamani ya shilingi Milioni 3.1 kwa ajili ya vituo vya kulelea watoto yatima mkoani Shinyanga ili kuhakikisha watoto wanaendelea kupata huduma ya chakula. 

Makabidhiano hayo ya chakula yamefanyika leo Ijumaa Disemba 4,2020 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. 

Vituo vya kulelea watoto yatima vilivyonufaika na msaada huo ni Shinyanga Society Orphanage Centre cha Mjini Shinyanga na Muvuma na Peace Kahama Orphanage Centre vya Mjini Kahama. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi chakula hicho, Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack aliwashukuru na kuwapongeza wasimamizi wa vituo vya kulelea watoto yatima kwa kazi kubwa wanayofanya kulea watoto. 

“Nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayofanya kwa kulea watoto. Hawa watoto ni wa kwetu, ni watoto wa Kitanzania, nyinyi mmejitoa kuhakikisha mnawasaidia waweze kupata maisha na pengine waweze kufikia ndoto zao. Tunaendelea kuwaombea kwa Mungu awape afya na umri,muweze kuendelea kufanya hiyo kazi”,alisema Telack. 

“Ndani ya mkoa huu tuna vituo vingi vya kulelea watoto,tuna Agape ACP ambao tayari tumeshawapa msaada wa vyakula wanaojihusisha kulea na kuwapa elimu watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia,tuna kituo cha Shinyanga Society Orphanage Centre kinacholea watoto wasio na wazazi”,aliongeza Telack. 

Aidha alitoa wito kwa wadau kujitokeza kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kwani watoto walitamani kuwa na wazazi lakini Mungu hakuwapa mapenzi hayo. 

“Watu hawa wamejitolea kulea watoto waliokosa wazazi,wengine hawana wazazi wote kabisa,yale mapenzi ya wazazi hawayapati. Yeyote atakayeguswa ajitokeze tusaidie hawa watoto”,alisema. 

“Katika kipindi tulichotoka cha Corona watu wengi waliokuwa wanasaidia wameondoa misaada yao na sisi kama mkoa tukaona tuangalie namna ya kusaidia ili watoto hawa waendelee kuishi,naomba wadau wajitolee ili kusaidia watoto hawa waweze kuishi na kuendelea kusoma wakiwa na mahitaji ya vifaa vya shule”,alisema Mkuu huyo wa Mkoa. 

Katika hatua nyingine aliwataka watoto wanaolelewa kusoma kwa bidii hususani watoto wa kike kuepuka vishawishi vinavyoweza kukatisha ndoto zao. 

Akipokea Chakula hivyo kwa niaba ya vituo vitatu vya kulelea watoto yatima, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kituo cha Shinyanga Society Orphans, Bi. Ayam Ally Said alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano anaoendelea kuwapatia kwa kutembelea kituo chake mara kwa mara na kutoa msaada wa vyakula na nguo. 

Alisema zaidi ya kupewa msaada wa chakula sasa wanahitaji msaada zana za kufanyia kazi wajitegemee ili watoto wafanye kazi, wawe watoto bora na baadaye kuwa wafanyakazi bora wa serikali. 

“Sisi Shinyanga Society Orphanage Centre hatuhitaji kuwa tegemezi hawa hatutawalea vizuri. Tunaomba kupewa zana za kufanyia kazi. Ombi langu kwa Mhe. Rais wetu Mpendwa Dk. John Pombe Magufuli tunaomba Trekta, maeneo tunayo, tunataka tujitegemee,hatulei watoto kama mayai”,alisema Ayam. 
Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akimkabidhi mchele Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kituo cha kulelea watoto yatima Mjini Shinyanga 'Shinyanga Society Orphans', Bi. Ayam Ally Said ili kuhakikisha watoto wanaendelea kupata huduma ya chakula katika kituo hicho leo Ijumaa Disemba 4,2020.  Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akimshukuru Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kituo cha kulelea watoto yatima 'Shinyanga Society Orphans', Bi. Ayam Ally Said kwa kuendelea kulea watoto yatima wakati akimkabidhi mchele ili kuhakikisha watoto wanaendelea kupata huduma ya chakula kituoni hapo.
Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akimshukuru na kumpongeza Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kituo cha kulelea watoto yatima 'Shinyanga Society Orphans', Bi. Ayam Ally Said na vituo vya Muvuma na Peace Kahama Orphanage  Centre kwa kujitolea kulea watoto yatima.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akiwaomba wadau kujitokeza kusaidia watoto wanaolelewa katika vituo vya kulelea watoto.
Kushoto ni Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kituo cha kulelea watoto yatima Mjini Shinyanga 'Shinyanga Society Orphans', Bi. Ayam Ally Said  akimshukuru Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack kwa ushirikiano anaotoa kwenye vituo vya kulelea watoto yatima.
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kituo cha kulelea watoto yatima Mjini Shinyanga 'Shinyanga Society Orphans', Bi. Ayam Ally Said akimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kukipatia  Trekta kituo chake kwa ajili ya kilimo kwani maeneo wanayo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Tedson Ngwale akielezea namna Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack anavyoendelea kusimama mstari wa mbele kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Muonekano wa magunia 17 (tani 1.7) ya mchele yenye thamani ya shilingi Milioni 3.1 yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack kwa ajili ya vituo vya kulelea watoto yatima mkoani Shinyanga ili kuhakikisha watoto wanaendelea kupata huduma ya chakula. 
Muonekano wa magunia 17 (tani 1.7) ya mchele yenye thamani ya shilingi Milioni 3.1 yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack kwa ajili ya vituo vya kulelea watoto yatima mkoani Shinyanga ili kuhakikisha watoto wanaendelea kupata huduma ya chakula. 
Muonekano wa magunia 17 (tani 1.7) ya mchele yenye thamani ya shilingi Milioni 3.1 yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack kwa ajili ya vituo vya kulelea watoto yatima mkoani Shinyanga ili kuhakikisha watoto wanaendelea kupata huduma ya chakula. 

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post