WAITARA ASEMA FEDHA ZA MGODI WA NORTH MARA SIYO ZA BURE,AKATAA MICHANGO ISIYO YA LAZIMA

 

Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara akizungumza jambo

Na Dinna Maningo - Tarime

Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini  Mwita  Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri mteule Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira amewataka Wenyeviti na Watendaji wa vijiji vinavyozunguka Mgodi wa North Mara kusimamia fedha za miradi zinazotolewa na Mgodi.

Mbunge huyo amezuia wananchi wanaozunguka mgodi kutochangishwa michango kwakuwa mgodi huo utoa asilimia moja ya fedha kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Waitara aliyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo iliyojengwa kwa fedha za Serikali chini ya mpango wa Lipa kulingana na matokeo (EP4R) na fedha za miradi ya uwajibikaji wa Mgodi kwa jamii (CSR).

Akiwa katika ukaguzi wa ujenzi wa Zahanati ya Komarera kata ya Nyamwaga utakaogharimu zaidi ya milioni 190, huku akiwa ameambatana na baadhi ya watendaji wa halmashauri,Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Simion Samwel,Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Victoria Mapesa na kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tarime.

"Fedha za mgodi si fedha za bure ni fedha ambayo ni asilimia moja ya mapato ya mgodi zinazokwenda moja kwa moja kwenye akaunti za vijiji kwa ajili ya kufanya miradi ya maendeleo,naomba muibue miradi ambayo ni muhimu kwa wananchi na muisimamie kusiwepo na ubadhilifu wa fedha hizo",alisema Waitara.


"Jambo kubwa lililokuwa linalalamikiwa ni michango ya Saiga (Rika) watu wanachangishwa fedha mtu hana wanamnyang'anya mali zake au kupigwa faini,watu wasichangishwe fedha isipokuwa kama kuna uhitaji muhimu,na wananchi washirikishwe kila hatua katika michango na matumizi ya fedha walizochanga", aliongeza Waitara.

Mbunge huyo  alikagua ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Tarime ambapo alihoji kutaka kufahamu sababu ya hospitali  hiyo kukosa dawa jambo ambalo limekuwa kero kwa wananchi na akaagiza halmashauri kuhakikisha ujenzi wa wodi za wagonjwa zinakamilika ili wananchi wapate huduma.

"Nashukuru ujenzi unaendelea vizuri ila Mkurugenzi hakikisha inakamilika kwa wakati  maana hii hospitali inategemewa na watu wengi ambao wako mbali na hospitali, mna ujenzi wa wodi 4 tunaapata changamoto kwa wananchi inapochelewa kukamilika na nimefurahi kila mradi ninaotembelea naambiwa fedha zipo.


Nimeambia hakuna dawa wala grovisi,naomba kujua kwanini hakuna dawa? kama kuna tatizo tujue ili tufanye utaratibu wa kupata dawa za dharura,tujitahidi kusaidiana hii ni huduma muhimu kwa watu",alisema Waitara.


Katibu wa afya halmashauri ya wilaya ya Tarime Sufian Mageta alikiri kutokuwepo kwa dawa nakwamba wodi zinazojengwa ni wodi ya wanawake na wanaume,wodi ya watoto,na chumba cha upasuaji.

"Awali hii ilikuwa ni zahanati dawa tulizokuwa tunazipata ilikuwa ni kwaajili ya zahanati na sasa taratibu za kimfumo zimefanyika tutapatiwa dawa ndani ya mwezi huu", alisema Mageta.

Waitara alikagua ujenzi wa madarasa shule ya msingi Soroneta kata ya Nyarero ujenzi unaogharimu sh.Milioni 60 ambapo mkuu wa shule hiyo Esther Nyeriga alisema kuwa ujenzi uko katika hatua za mwisho za ukamilishaji.

Wa kwanza kulia ni mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa  wakiwa kwenye ukaguzi wa kituo cha afya Magoma kata ya Binagi


Mbunge Mwita Waitara akiteta jambo na katibu wa afya hospitali ya wilaya ya Tarime Sufian Mageta  wa kwanza kulia
Ujenzi wa zahanati ya Komarera
Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara akizungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Komarera wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho
Baadhi ya majengo hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Tarime

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments