MWANAUME ALIYEPIGANA NA MKE WAKE ATEMBEA KWA MIGUU WIKI NZIMA KUTULIZA HASIRA


Mwanaume Muitalia alitoroka nyumba yake ili kutuliza jazba baada ya kupigana na mke wake  kwa kusafiri wiki nzima mwendo wa kilomita 450 kwa miguu.

Mitandao ya kijamii ya Italia haka imempa jina la "Forrest Gump" kutoka filamu ya Tom Hanks ya mwaka 1994, ambaye alisafiri maili elfu kadhaa nchini Marekani.

Polisi walimzuia alipokuwa akikimbia majira ya saa nane za usiku katika eneo la Fano nchini humo, baada ya kuondoka nyumbabi kwake katika jimbo lililoko kaskazini mwa Italia.

Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 48- alipigwa faini na polisi kwa kuvunja amri ya kutotoka nje.

Taarifa kumuhusu mwanaume huyu ilitolewa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Resto del Carlino lililopo katika jimbo la Bologna , na mara moja zikachapishwa katika vyombo vya habari vyote kote nchini Italia.

Watu wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu kisa hicho kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi wakimuita mwanaume huyo shujaa na wengine wakipinga kitendo chake cha kumtoroka mkewe na kukimbia ovyo badala ya kukaa naye na kutatua mzozo wao kwa amani.

Baadhi walisema kuwa anapaswa kupewa tuzo la heshima pia-lakini wengine walisema hayuko sawa. Wengine walimsifu kwa kuamua kutoka nyumbani mwake ili kutuliza hasira yake badala ya kusababisha matatizo.

Mwanaume huyo alisema "Nilikuja hapa kwa miguu, sikupanda gari." "Njiani nilikutana na watu ambao walinipatia chakula na maji . Nilishiba lakini nilichoka," anasema alitembea mwendo wa kilomita 60 kwa siku.

Polisi walimpata usiku akiwa amepigwa na baridi kali alipokuwa akitembea barabarani.

Baada ya kuchunguza kitambulisho chake, waligundua kuwa mke wake alikuwa ametoa tangazo kwamba alikuwa amepotea. 

Waliwasiliana na mke wake mara moja na akaja kumchukua katika eneo la Fano ambako alipelekwa na polisi.

Chanzo - BBC Swahili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post