TIMU YA WASICHANA U-17 YAREJEA NCHI NA UBINGWA COSAFA

Kikosi cha timu ya Taifa ya Wasichana chini ya umri wa miaka 17 ‘Tanzanite Queens’ kimetua hapa nchini usiku wa kuamkia leo wakitokea nchini Afrika Kusini ambapo walifanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA).

Tanzania ilitwaa ubingwa huo baada ya kuwafunga Zambia kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Nelson Mandela Bay baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya goli 1-1.

Katika mchezo huo, Zambia walikuwa wa kwanza kupata goli lililofungwa dakika ya 19 na mshambuliaji Comfort Seleman ambaye alitumia vizuri makosa ya safu ya ulinzi ya Tanzania baada ya kuondoka na mpira kuanzia katikati ya uwanja hadi kwenye goli na kupiga shuti  ambalo lilimsinda golikipa Aisha Mrisho.

Lakini kipindi cha pili Tanzania ilisawazisha bao hilo kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Koku Kipanga baada ya Aisha Masaka kuchezewa madhambi ndani ya eneo la 18 na mchezo huo kumalizika kwa sare ya goli 1-1.

Akizungumza mara baada ya kuipokea timu hiyo, Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallece Karia amesema kuwa, wakati timu hiyo inaondoka aliwataka wachezaji hao pamoja na wale wa timu ya wakubwa, Twiga Stars kuhakikisha mmoja wao wanarudi na kombe hilo ikiwa kama zawadi kwa viongozi wapya wa serikali waliopata ushindi wa kishindo.

Amesema, anafurahi kwa kuwa timu hiyo imekuwa ya kwanza kutoa zawadi ya ushindi kwa viongozi hao na jambo kubwa kwa sasa ni kuomba kupata sapoti kwaa ajili ya vijana hao wa kike na kiume kwani ndio msingi wa timu nzuri za Taifa kwa miaka ijayo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments