TASAF YAANZA AWAMU YA PILI YA UHAKIKI WA WALENGWA


Mkurugenzi wa Programu za Jamii-TASAF Amadeus Kamagenge(aliyesimama) akifungua kikao kazi cha Wawezesha wa kitaifa wa zoezi la kuhakiki Walengwa waTASAF ,kulia kwake ni meneja wa Masjali ya walengwa wa TASAF,Bi. Phillipine Mmari na kushoto ni Mtaalamu wa Mafunzo Bi. Mercy Mandawa.
Baadhi ya Wawezeshaji wa kitaifa wa zoezi la Uhakiki wa Walengwa wa TASAF,wakiwa kwenye ukumbi wa ofisi ndogo ya TASAF jijini Dar es salaam wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa kikao kazi hicho iliyotolewa na Mkurugenzi wa Programu za Jamii Amadeus Kamagenge (hayupo pichani).

Na Estom Sanga-TASAF 

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF umeanza awamu ya pili ya zoezi la uhakiki wa Walengwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alilolitoa wakati wa uzinduzi wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF mwanzoni mwa mwaka huu jijini Dar es salaam. 

Akifungua kikao kazi cha Wawezeshaji wa kitaifa kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ndogo ya TASAF jijini Dar es salaam, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Ladislaus Mwamanga,Mkurugenzi wa Programu za Jamii Amadeus Kamagenge amesisitiza umuhimu wa kutekelezaji zoezi la uhakiki wa Walengwa kwa umakini mkubwa ili kuondoa uwezekano wa kuwa na walengwa wasiostahili kunufaika na huduma za Mpango. 

‘’Uhakiki na uandikishaji sahihi wa Walengwa ndiyo Msingi wa kuwapata Walengwa sahihi wa kuhudumiwa kwenye Mpango’’ amesisitiza Kamagenge. 

Amesema licha ya mafanikio makubwa katika utekelezaji wa shughuli za Mpango ,TASAF imeweka uzito mkubwa kwenye zoezi la uhakiki wa Walengwa ili wanaokidhi vigenzo ndio wanufaike kama ilivyoagizwa na serikali. 

Akitoa maelezo ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya zoezi la uhakiki wa Walengwa ,Meneja wa masjala ya Walengwa wa TASAF ,Bi.Phillipine Mmari amesema asilimia 80 ya Walengwa walihakikiwa katika awamu hiyo iliyofanyika kote nchini. Na asilimia 20 watahakikiwa katika zoezi litakalofanyika katika awamu ya pili. 

Serikali kupitia TASAF inatekeleza kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambacho kinatarajiwa kuhudumia takribani Kaya milioni MOJA na Laki NNE ili kuwawezesha wananchi wanaoishi katika umaskini uliokithiri kupata fursa ya kukuza kipato na kuboresha miundombinu katika sekta za elimu,afya na maji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post