SERIKALI YAWAONYA WAMILIKI WA MADUKA YA DAWA


 SERIKALI imewataka wamiliki wa maduka ya dawa za binadamu kuacha kutoa dawa kwa mgonjwa ambaye hana cheti cha daktari/tabibu kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria zilizowekwa.
Pia imewaomba wananchi kuhakikisha wanatumia dawa kwa uangalifu na umakini zaidi ili kuweza kuepuka usugu wa vimelea dhidi ya dawa aina ya Antibayotiki.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es salaam jana na Mganga Mkuu wa serikali Profesa Abel Makubi alipokuwa akizindua maadhimisho ya wiki ya kuamasisha wananchi kuhusu uelewa wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa aina ya Antibayotiki.

Alisema baadhi ya maduka ya dawa yamekuwa yakifanya makosa kwa kumpatia mgonjwa dawa bila ya kuona cheti kilichotolewa na daktari.

“Cheti cha daktari ni muhimu kwa mgonjwa kuwanacho kabla kupewa dawa ya aina yoyote iwe katika kituo cha huduma ya afya au duka la dawa”alisema Profesa Makubi

Alisema kutolewa kwa dawa hizo kiolela bila ya kuona cheti cha daktari kinaweza kumsabisha mgonjwa usugu wa vimelea vya dawa.

Alisisitiza kuwa uwepo wa usugu wa vimelea vya katika dawa Antibayotiki unaweza kuliweka taifa katika kupoteza nguvu kazi pamoja na kutumia fedha nyingi kutumia kununua dawa

Profesa Makubi alisema kutokana na matumizi mabaya ya dawa hizo kwa tiba ya binadamu na wanyama madhara yake yamekuwa makubwa ya kutisha.

Alisema kwa mujibu wa tafiti zimeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa za matumizi ya dawa hizo kutumika isivyo sahihi.

” Asilimia 50 ya dawa zimekuwa zikitumika isivyo sahihi huku matumizi makubwa kutibia mifugo na kuchaganywa katika vyakula vya wanyama kinyume na taratibu za kitabibu”alisema Profesa Makubi

Aliongeza kuwa ripoti ya benki ya dunia ya mwaka 2017 inabainisha kuwa zaidi ya watu laki 7 wanafariki Kila mwaka kutokana na usugu wa dawa hizi.

Akizungumza kuhusu utumiaji wa dawa kwa mgonjwa alisema anapaswa kufuata maelekezo ya dawa sahihi ikiwa ni pamoja na kuepuka kukatisha dozi.

” Kila mtu anapaswa kufuata matumizi sahihi ya dawa ikiwa ni pamoja na kutozitumia kiolela ikiwa ni pamoja na kutokukatisha dozi “alisema Profesa Makubi

Kwa upande wake Mfamasia Mkuu wa serikali Daud Msasi alisema kwa sasa wanafanya utaratibu wa kupitia maduka yote Kama njia ya kujiridhisha katika utoaji wa dawa.

Aidha alitaka jamii kuacha kutumia dawa ambazo mtu tayari amezitumia kwani kufanya hivyo kinaweza kusababisha usugu wa dawa.

Pia alisema kupitia wiki hii wanaendelea kutoa elimu ya uelewa juu ya matumizi sahihi ya dawa aina ya Antibayotiki ili siweze kusababisha vimelea vya usugu dhidi ya dawa hizo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post