RAIS MAGUFULI: UCHAGUZI UMEKWISHA, SASA NI MUDA WA KULIJENGA TAIFA LETU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Magufuli  amewaeleza wananchi wa  Tanzania kuwa uchaguzi mkuu umemalizika na jukumu lililopo mbele ni kuwatumikia wananchi.

Rais Magufuli amesema hayo leo Alhamisi tarehe 5 Novemba 2020 baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma kuwa Rais wa Taifa hilo, sherehe iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Pia, Samia Suluhu Hassan, ameapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania ambao kwa pamoja watawaongoza Watanzania kwa kipindi kingine cha miaka mitano 2020-2025.

Dk. Magufuli ameapishwa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mshindi wa urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano ya tarehe 28 Oktoba 2020 kwa kupata kura milioni 12 kati ya milioni 15 zilizopigwa sawa na asilimia 84.

Rais Magufuli amewashukuru watu mbalimbali waliojitokeza kwenye sherehe hizo, “nawashukuru sana na mimi kuwa Rais wa kwanza kuapishwa katika hili Jiji la Dodoma.”

Huku akishangiliwa, Rais Magufuli amesema “nawashukuru Watanzania wenzangu kwa kuniamini na kunichagua ili niwaongoze kwa miaka mitano na kukipa ushindi mkubwa chama changu cha mapinduzi na ushindi huu si wa wana CCM pekee bali ni wa Watanzania wote”

Pia, ameipongeza, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kusimamia uchaguzi huu pamoja na kuvishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kudumisha amani kabla na baada ya uchaguzi.

Rais Magufuli amesema, baadhi ya nchi, uchaguzi umekuwa chanzo cha mgogoro na uhasama, “sisi Watanzania tumevuka salama na hii ni ishara kwamba mwenyezi Mungu ametuvusha salama kama alivyotuvusha kwenye janga corona.”

“Nawashukuru viongozi wa mataifa mbalimbali waliokuja kuungana nasi, wapo marais, mawaziri wakuu, mawaziri na mabalozi wote na wawakilishi wa taasisi za mataifa kama EAC na SADC,” amesema Rais Magufuli.

Kiongozi huyo amesema “uchaguzi sasa umekwisha, uchaguzi sasa umekwisha, uchaguzi sasa umekwisha na jukumu kubwa na muhimu lililopo mbele ni kulijenga na kuleta maendeleo taifa letu na niwahakikishe Watanzania, kiapo nilichoapa na makamu wangu (Samia Suluhu Hassan), tutakienzi.”

Rais Magufuli amesema, katika uongozi wa miaka mitano, watasimamia kumaliza miradi waliyoianzisha, kusimamia rasilimali mbalimbali za taifa, kushughulikia tatizo la ajira hususan vijana na kero zinazowakabili wananchi na kuzidisha mapambano ya rushwa na ufisadi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments