RAIS MAGUFULI: KAZI YA UWAZIRI MKUU HAINA GUARANTEE, ITATEGEMEA NA UTENDAJI WAKE


 Rais Dkt. John Magufuli ameendelea kuiunda serikali yake ya muhula wa pili ambapo leo amemuapisha Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu, Prof. Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Dkt. Philip Mpango kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ikiwa ni hatua za kuendelea kukamilisha baraza la mawaziri.

Akizungumza baada ya kuwaapisha wateule hao, Rais Magufuli amewataka wafanye kazi mara mbili ya walivyokuwa wanafanya katika muhula wa kwanza kwani kipindi hiki hakuna raha na uteuzi wao utategemea na utendaji wao.

Akitolea mfano wa Waziri Mkuu, amesema amona watu mkoani Lindi wakishangilia kuwa wametoa Waziri Mkuu kwa miaka mingine mitano, lakini yeye akasema kazi hiyo haina dhamana kwamba aliyeteuliwa lazima atakaa miaka mitano.

“Waziri Mkuu nikupongeze sana kwa nafasi hii, nilikua naangalia mawaziri wakuu wenzako waliopita muda waliokaa nikaona nikuteue haraka haraka sasa sijui nilipatia? Maana Nyerere alikaa mwaka mmoja, Kawawa mitatu, Sokoine mitatu, Msuya mitano, Sokoine akarudi akakaa mwaka mmoja tena, Dk Salim akakaa mwaka mmoja, Warioba mitano, Malecela minne na Msuya akarudi kukaa mmoja, Sumaye yeye ndio alikaa miaka 10 yote, Lowassa mitatu na Pinda saba. Hivyo ndugu zangu nataka muelewe kuwa nafasi ya uwaziri mkuu siyo ya 'guarantee' sana itategemea na ufanyaji kazi wake hivyo umuombe sana Mungu na wabunge pia mumuombee ili aweze kufikia rekodi ya Sumaye na Mama Majaliwa pia uelewe una kazi ya kumuombea ," Amesema Dk Magufuli.

Amesema kuwa amezunguka nchi nzima na wananchi wamemuamini kwa kumpa kura za kishindo, hivyo kura hizo lazima zionekane katika yale ambayo serikali itayafanya.

“Imani waliyoitoa kwa Chama cha Mapinduzi ni lazima tukaitimize kwa nguvu zote,” amesisitiza Magufuli.

Dkt. Magufuli amesema amelazimika kuanza na wizara hizo mbili kwa sababu masuala ya fedha hayawezi kusubiri hadi ateue baraza zima, na kwamba waziri wa mambo ya nje ni muhimu ili awepo mtu wa kuisemea nchi kimataifa muda wote.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post