MAJALIWA : ELIMUMSINGI BILA ADA IMEONGEZA UFAULU NCHINI

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema kiwango cha ufaulu nchini kimeongezeka kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 iliyoielekeza Serikali kutoa elimumsingi bila ada.

Amesema Serikali ya CCM imetumia shilingi trilioni 1.09 kugharamia elimumsingi bila ada kwa shule za msingi na sekondari ambapo shule mpya za msingi 905 zimejengwa na sekondari 228 nchi nzima, pia shule kongwe 73 zimekarabatiwa pamoja na ujenzi wa mabweni mapya 253 na maabara 227.

Aliyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Oktoba 8, 2020) wakati alipozungumza na wananchi kwa nyakati tofauti katika kata za Songe na Kwediboma wilayani Kilindi na kata ya Chanika wilayani Handeni, Tanga katika mikutano ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt Magufuli.

Alisema kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza imeongezeka kutoka milioni moja mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa wanafunzi milioni 1.6. Pia Serikali imefuta michango yote ya hovyo waliyokuwa wakitozwa wanafunzi ikiwemo ya kuchangia huduma ya maji na ulinzi.

Akizungumzia kuhusu fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kugharamia elimumsingi bila ada katika halmashauri ya wilaya ya Kilindi, Mheshimiwa Majaliwa alisema jumla ya shilingi bilioni 2.64 zilitolewa kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa Maofisa Elimu Kata na Walimu Wakuu.

Mheshimiwa Majaliwa Alisema jumla ya shilingi bilioni 1.82 zilitolewa na Serikali kwa shule 22 za sekondari wilayani Kilindi kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule, hivyo amewaomba wananchi wawachague viongozi wa CCM kwani wanamikakati mizuri ya kuwaletea maendeleo.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa aliwaeleza wakazi wa Handeni kwamba Serikali yao itaendelea kuwatumikia na kuboresha huduma za jamii zikiwemo za elimu, maji na afya. Alisema Serikali imetoa sh. milioni 83.8 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya Hospitali ya Wilaya Handeni. “Kazi inaendelea na katika bajeti ya 2020/2021 hospitali hiyo imetengewa sh. bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Katika kipindi miaka mitano ijayo CCM inalenga kuimarisha ubora wa elimu katika ngazi zote kwa kuzingatia falsafa ya kujitegemea yenye kuendana na mazingira ya nchi, hususan elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na katika kutimiza azma hiyo, Chama kitaielekeza Serikali kushirikiana na sekta binafsi, asasi za kiraia zikiwemo taasisi za dini katika kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu na ujuzi.

Pia CCM imeielekeza Serikali kupitia Ilani iimarishe idara na taasisi za udhibiti ubora zikiwemo NACTE, TCU na Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule ili kuhakikisha kwamba kiwango cha ubora wa elimu itolewayo nchini kinazingatiwa na kuimarika pamoja na kuimarisha misingi ya elimu ya kujitegemea katika ngazi zote za elimu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments