Dkt. Magufuli: Ahadi Zote Zilizotolewa Kuhusu Pemba Zitatekelezwa


MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wananchi wa kisiwa cha Pemba kuwa ahadi zote zilizoandikwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 kuhusu miradi na mipango ya maendeleo kisiwani humo zitashughulikiwa kwa ushirikiano kati yake na mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt Hussein Ali Mwinyi endapo watachaguliwa.

Ameyasema hayo jana (Jumanne, Oktoba 13, 2020) alipozungumza na wakazi wa Kisiwa cha Pemba kupitia simu aliyompigia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Mchangamdogo Kambini katika jimbo la Kojani, Kaskazini Pemba.

Mheshimiwa Dkt. Magufuli ameahidi kufanya kazi kwa karibu na kumpa ushirikiano wa hali ya juu Dkt. Mwinyi endapo atachaguliwa kuwa Rais na lengo likiwa ni kuleta maendeleo ya haraka na makubwa katika visiwa vya Unguja na Pemba.

“…Nimemtuma Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa afanye kazi moja ya kwanza ni ya kuniombea kura mimi John Joseph Magufuli, mtanipa lakini? la pili nataka nimuombee kura Mheshimiwa Mwinyi awe Rais wa Zanzibar na wawakilishi na madiwani hapo Pemba muwape wote wa kutoka CCM. Ninataka niwahakikishie changamoto zenu mlizonazo za maji, ajira na masuala mbalimbali zitashughulikiwa msipoteze kura zenu muniletee Mwinyi.”

Pia, Mheshimiwa  Dkt. Magufuli amemuagiza Mheshimiwa Majaliwa ampelekee orodha ya miradi na mipango ya maendeleo iliyotajwa katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 pamoja na mambo yote ambayo Dkt. Mwinyi ameyatolea ahadi katika mkutano huo na kwamba atatoa ushirikiano ili kuhakikisha ahadi hizo zinatekelezwa,

Amewasihi wananchi wa Pemba wasifanye makosa tena katika uchaguzi ujao bali wawachague wagombea wa CCM katika nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani, hatua ambayo italeta ushirikiano mzuri kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano na Zanzibari na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye, Mheshimiwa Majaliwa amewapongeza wananchi wa Pemba kwani wameonesha wazi kuwa wamebadilika, wamechoka kudanganywa na sasa wapo tayari kuipigia kura CCM, hivyo amewasisitiza wamchague Dkt. Mwinyi ambaye ni muadilifu na ameahidi kuunda Serikali itakayowatumikia wananchi kwa kukusanya na kusimamia mapato na mali za Serikali.

“Nawasihi sana ndugu zangu tumchague Dkt. Mwinyi ili aweze kupambana na wala rushwa na mafisadi, akiunganisha nguvu zake na Serikali ya Muungano wa Tanzania ataweza kuifanya Zanzibar ipae kiuchumi.”

Mheshimiwa Majaliwa amewasihi sana wasikubali kutumika vibaya katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuchagua viongozi wasioaminika kwa sababu tu za ushabiki wa kisiasa badala yake wamchague Dkt. Mwinyi ambaye amedhamiria kuwaletea maendeleo Wazanzibar wote na kutatua kero zao.

Kwa upande wake, mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dkt. Mwinyi amesema Muungano wetu ndio utakaotuletea maedndeleo na si kinyume chake. Ametaja faida za Muungano kuwa ni pamoja na amani na utulivu na kwamba ili waendelee kuwa na amani lazima Muungano huo uendelee kuwepo. “Juhudi zote na mipango mizuri ya maendeleo na maisha bora kwa Wazanzibar hazitofanikiwa kama amani itatoweka.”

Awali, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Balozi Seif Ali Idd amewahakikishia Wazanzibar kuwa Serikali itaimarisha ulinzi siku ya uchaguzi ambayo ni Oktoba 28 mwaka huu, hivyo wasikubali kudanganywa na wanasiasa wasioitakia mema Zanzibar kwenda kupiga kura siku ya Oktoba 27, ambayo ni maalumu kwa ajili ya vikosi vya ulinzi na usalama.

 (mwisho)  Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments