CHEMBA YAHAMASIKA NA MAFUNZO KILIMO CHA KOROSHO


Mkuu wa Wilaya ya Chemba Simon Chacha
akizungumza na Wanahabari kuhusiana na programu ya mafunzo ya kilimo bora cha zao la korosho yanayoendelea kutolewa na Kituo cha TARI Naliendele kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho kwenye mikoa ya Kanda ya Kati, ikiwemo
Halmashauri ya Chemba.

 Maafisa Ugani na Wakulima kuzunguka wilaya ya
Chemba wakiwa kwenye mafunzo hayo.
   
Mafunzo yakiendelea.


Na Godwin Myovela, Chemba
MKUU wa Wilaya ya Chemba Simon Chacha amesema mafunzo ya Kilimo Bora cha Korosho yanayoendelea kutolewa kwenye mikoa 17 nchini ikiwemo Chemba yamekuja wakati mwafaka, na kwamba yatakuwa kichocheo kikubwa cha maboresho ya zao hilo muhimu kuendana na mahitaji ya soko sambamba na kuchangia kasi ya mabadiliko ya kiuchumi kwa mkulima na jiografia ya sehemu husika.

Akizungumza na wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI)-kupitia Kituo chake cha Naliendele ofisini kwake juzi, Chacha alisisitiza kwamba sasa kuna kila dalili njema ya chemba kuanza kupaa kiuchumi kupitia zao hilo baada ya kufikiwa na mafunzo hayo.

“Tunawashukuru TARI na Bodi ya Korosho kwa kufika Chemba kwa ajili ya kutupa teknolojia za kisasa za uzalishaji bora wa zao hili. Hapa kwetu hali ya hewa ni nzuri na udongo wake unafaa kustawisha korosho, tunaamini mafunzo haya kupitia wakulima na maafisa ugani yatakwenda kuboresha kilimo chetu kuwa na tija zaidi,” alisema Mkuu wa Wilaya.

Awali, Mtafiti Mwandamizi na Mratibu wa zao hilo kitaifa kutoka TARI Naliendele, Dk.Geradina Mzena alisema Chemba ni miongoni mwa maeneo rafiki sana kwa zao hilo.

Awali, Mtafiti Mwandamizi na Mratibu wa zao hilo kitaifa kutoka TARI Naliendele, Dk Geradina Mzena alisema Chemba ni miongoni mwa maeneo rafiki sana kwa zao hilo maarufu ‘Dhahabu ya Kijani’ huku akiwasihi wana-chemba kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo na kuongeza wigo wa mashamba, na serikali ipo bega kwa bega kuhakikisha inawapa utaalamu wote unaohitajika.

Mzena alisema kwa sasa serikali kupitia TARI imejipanga kuzalisha miche zaidi ya milioni 22 (tani 150) ya mbegu bora za korosho kwa msimu huu ambayo itasambazwa kwa wakulima kwa utaratibu maalumu wa kimfumo baada ya mkulima kukamilisha taratibu na kupatiwa namba ya malipo kutoka kwenye taasisi hiyo.

“Korosho ni utajiri, korosho ni zao la kimkakati, mbegu zake ni salama na lina uhakika wa soko. TARI tuna aina 54 za mbegu bora za zao hili tulizozifanyia utafiti na kuthibitika kuwa na ubora unaohitajika kwenye soko, pia mbegu tunazozalisha zinakinzana na mashambulizi ya magonjwa na wadudu waharibifu,” alisema Mzena na kuongeza:

“Tumetoa punguzo la hadi shilingi elfu tano kwa kilo moja ya mbegu, na kilo moja unapata kuanzia miche mia moja na hamsini. Hii ni fursa kubwa kwa wakulima kwa sababu mbegu hizi mavuno yake ni bora sana,” alisema. 

Serikali kupitia TARI Naliendele mpaka sasa inaendelea kutoa mafunzo kwa maafisa ugani na wakulima wa korosho kwenye mikoa 17 inayolima zao hilo, lengo ni kuongeza tija ya uzalishaji wake ili kuleta matokeo chanya ya kiuchumi kwa mkulima na Taifa kwa ujumla.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527