DC KISWAGA ATAHADHARISHA MAGONJWA YA MLIPUKO MACHIMBONI


Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga.

Na Sitta Tumma,Bariadi.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu, Festo Kiswaga, ameonya uchafuzi wa kimazingira katika machimbo ya dhahabu ya Gasuma, akisema hali hiyo isipodhibitiwa inaweza kusababisha kutokea magonjwa ya mlipuko.

Ametaka wafanyabiashara wa vyakula na bidhaa mbalimbali eneo hilo la kiuchumi, kutilia mkazo usafi.

DC Kiswaga amesema hayo alipozuru eneo la mgodi huo, ambapo alizungumzia mambo kadhaa ya kiusalama, uchumi na tahadhari ya magonjwa ya mlipuko kwenye maduara hayo.

 "Nataka mzingatie suala usafi. Sitaki milipuko ya magonjwa itokee kwa sababu ya uchafu unaozuilika.

"Ikitokea, huu mgodi nitaufunga," DC Kiswaga ameonya huku akitaka kulindwa kwa mazingira.

Sheria ya Tanzania inayoangazia masuala ya Mazingira ya mwaka 2004, pamoja na mambo mengine inataka kila mtu kulinda mazingira.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wilaya ya Bariadi, kila mtu anatakiwa alinde mazingira kwa ajili ya afya.

Amesema Serikali haihitaji kupoteza nguvukazi kwa sababu ya magonjwa.

"Magonjwa ya mlipuko ni hatari katika uchumi wa familia, mtu na Serikali.

"Tulindeni mazingira," amesisitiza DC Kiswaga, akitaka pia maafisa afya na mazingira watimize vema wajibu wao.

Kulingana na kiongozi huyo anayeegemea pia masuala ya kilimo, kila mtu ana wajibu wa kudhibiti mazingira.

Taarifa mbalimbali zinadai kuwa, zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaofika kwenye vituo vya kitabibu, wanasumbuka na magonjwa yatokanayo na uchafuzi wa kimazingira.

Moja ya Ajenda Kuu zinazoangaziwa na  Umoja wa Mataifa (UN) zinaelekea kwenye usalama wa kimazingira.

Ripoti ya wataalamu wa masuala ya mazingira iliyotolewa katika Kikao cha Baraza la Mazingira Ulimwenguni, mwaka jana, jijini Nairobi, Kenya, imeonya kuhusu hatari ya uchafuzi wa mazingira wenye madhara ya kiafya dhidi ya binadamu.

Katika Kikao cha Baraza hilo, kilichoketi mwaka 2018, Nairobi, ilielezwa kuna uwezekano wa Ziwa Victoria kujaa takataka ifikapo mwaka 2050, iwapo uchafuzi wa mazingira utaendelea kuwa sinema. 

Baraza hilo lilikaririwa likisema: "Samaki katika Ziwa Victoria watapotea ifikapo mwaka 2050, endapo udhibiti wa mazingira utagonga mwamba." 

Daktariuala ya binadamu, Dk. Hamis Kulemba, anayehudumu Mkoa wa Simiyu, anasema wanataka kuona ukuaji wa uchumi na si jamii yenye mserereko wa afya.

"Kipaumbele chetu ni maendeleo," amesema Dk. Kulemba, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Bahame Sandula, mkazi wa Gasuma, amehoji sababu ya maeneo ya migodi kutakata uchafu.

"Hatupendi magonjwa. Maafisa afya lazima wawajibike kuhimiza usafi na utunzwaji mazingira," amesema.

Nchambi Ndulu, yeye ameomba ukaguzi kufanyika mara kwa mara maeneo ya mikusanyiko ya watu, ili kuinusuru jamii uwezekano wa kutumbukia kwenye magonjwa ya mlipuko.

Afisa mmoja anayehusika na mambo ya afya wilayani Bariadi, ametaka jamii yoye kujiepusha na changamoto ya uchafuzi mazingira.

"Afya ni muhimu. Ndiyo mtaji wa mwanadamu....magonjwa ya milipuko yanaua. Yapaswa kudhibitiwa," amesema Sakina Mlawa.

Kulingana na hayo, wananchi inawalazimu kuishi kwa kuzingatia kanuni za afya, ili kujiweka pembezoni na magonjwa ya mlipuko.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments