WAKULIMA 439 MKOANI TABORA WANUFAIKA NA KADI ZA BIMA ZA AFYA

NA TIGANYA VINCENT
JUMLA ya wakulima 439 wananufaika na mpango wa bima ya afya kwa wakulima inayotolewa na Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya.

Kauli hiyo imetolewa jana wilayani Igunga na Mkurugenzi Mkuu Bernard Konga wakati wa uzinduzi wa mpango wa Bima ya afya kwa wakulima kwa kushirikiana na benki ya TPB kupitia mpango wa ushirika afya .

Konga alisema kupitia mpango huu, Benki ya TPB itakuwa na akaunti za wakulima hawa ambazo zitatumika kwa ajili ya malipo ya mauzo ya mazao yao.

Alisema Benki ya TPB itawalipia wakulima mchango wa bima ya afya wa mwaka ambao ni Shilingi 76,800 na mkulima atapata kadi ya bima ya afya ambayo ataitumia na kupata huduma za matibabu ndani ya Tanzania katika vituo zaidi ya 8,900 vya Serikali na binafsi vilivyosajiliwa kuhudumia wanachama wa Mfuko.

Alisema mkulima huyu anaruhusiwa pia kusajili mwenza wake na wategemezi wake kwa kumchangia kila mmoja kiasi hicho na kama ni mtoto wa chini ya miaka 18 atamchangia Shilingi 50,400 kwa mwaka.

Aidha Konga alisema hadi kufikia Mwezi  Juni mwaka huu, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulikuwa na jumla ya wanufaika 4,403,581 sawa na asilimia 8 ya watanzania wote.

Alisema hali hiyo inaonesha kwamba bado kuna kazi kubwa ya kutoa elimu kwa umma kuhusu dhana na umuhimu wa kuwa na bima ya afya.

Konga aliongeza watazidi kupanua  mpango huo na  kufikia wakulima wengi wa pamba na wa mazao mengine.

Akizindua mpango huo Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati aliitaka Ofisi ya Mrajis kuendelea kuwahimiza wakulima katika vyama vyao kujiunga na bima ya afya ili waweze kupata unafuu wa matibabu.

Alisema mpango huo ni suluhisho kubwa kwa wakulima kwani watakuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wote hata kabla ya kupokea mapato ya mauzo ya mazao yao.

Dkt. Sengati aliimiza Benki ya TPB na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhakikishai wanawafikia wakulima wa mazao yote nchini kwa utaratibu huo badala ya kuishia kwa wakulima wa pamba tu.

Aliwataka Wakulima waliopata vitambulisho kuwa wajumbe katika mpango huu kwa kuwahamasisha wengine kujiunga ili kila mmoja awe na unafuu wa huduma za matibabu.

Mwisho


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527