NHIF, TPB WAZINDUA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WAKULIMA WA PAMBA IGUNGA


WADAU wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wametakiwa kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Mfuko huo katika kuingiza makundi mbalimbali ya wananchi katika huduma zake ili kutimiza ndoto ya Serikali ya bima ya afya kwa wote.

Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mwamashimba wilayani Igunga, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Phillemon Sengati wakati wa uzinduzi wa mpango wa bima ya afya kwa wakulima wa zao la pamba, alisema “Utaratibu huu wa bima ya afya ni suluhu kubwa ya kila mkulima kuipatia kaya yake uhakika wa matibabu wakati wowote,” alisema.

Alisema kuwa endapo wakulima wataitumia fursa hiyo vizuri itawapa ufanisi katika uzalishaji mali kwani wakati wote mkulima anakuwa na amani lakini pia mapato yake yatatumika kwa maendeleo na sio kulipia huduma za matibabu.

Uzinduzi huo wa mpango wa bima ya afya kwa wakulima, ulifanyika kwa ushirikiano wa NHIF na TPB Benki ambayo inawakopesha wakulima hao fedha za mchango bila ya kuwa na riba yoyote ambapo fedha hizo watazilipa baada ya kuuza mazao yao.

“Nimeambiwa kuwa fedha zinazotolewa na TPB benki hazina makato wala riba yoyote hivyo ni jambo ambalo limelenga kumkomboa mkulima na kumhakikishia uhakika wa kupata matibabu wakati wowote,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuihimiza ofisi ya Mrajis ambayo ni msimamizi wa vyama vya ushirika kutumia nafasi yake kuendelea kuwahimiza wakulima katika vyama vyao kujiunga na bima ya afya na hasa kwa taratibu hizi zilizorahisishwa.

“Nanyi NHIF hakikisheni mnawafikia wakulima wa mazao yote nchini ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wote lakini pia tumieni fursa ya kushirikiana na wadau kama mabenki ili kufanikisha taratibu rahisi za uchangiaji na Benki ya TPB najua mmeanza na wakulima hawa wa pamba, nawahimiza mpanue wigo na kuwajumuisha wakulima wa mazao mengine pia ili wanufaike na utaratibu huu,” alisema Mkuu wa Mkoa.

Alitumia fursa hiyo pia kuwaagiza Watoa huduma kuhakikisha wanatoa huduma nzuri kwa wanachama wa NHIF ili waone faida ya kuwa ndani ya mfumo wa bima ya afya na akaweka msimamo wake wazi kuwa ndani ya Mkoa wa Tabora hatamvumilia mtoa huduma yoyote ambaye atahudumia wanachama na wananchi kinyume cha maadili.

“Utaratibu wa Bima ya Afya ndio mtindo bora wa sasa haya mambo ya kupenda kupokea fedha taslimu na kutoa lugha za kukera kwa wagonjwa halitakubalika ndani ya Mkoa wangu hivyo ni vyema mkajielekeza kutoa huduma nzuri kwa wananchi na wanachama ambao wamechanguia fedha zao kabla ya kuchangia,” alisema.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mpango huu, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga aliweka wazi kuwa, Mfuko umejipanga kuhakikisha unawahudumia kikamilifu wakulima ili wawe na uhakika na shughuli zao za kilimo katika kipindi chote cha mwaka.

“Lengo kubwa la mpango huu ni kuwawezesha wakulima wawe na uhakika wa afya zao kwa maana ya kupata huduma za matibabu wakati wowote wanapozihitaji na kwa upande wa Mfuko tumeboresha zaidi huduma zetu ili mwanachama wetu asipate usumbufu wa aina yoyote,” alisema Bw. Konga.

Naye Mkurungenzi Mtendaji wa Benki ya TPB, Bw. Sabasaba Moshingi alisema “Afya ya wateja wa benki ni muhimu sana katika kuwawezesha kufanya shughuli zao za kila siku hivyo mpango huu wa bima ya afya kwa wakulima wa zao la Pamba utachochea afya imara kwa wateja wa benki na kuweza kuchangia katika shughuli zao za kiuchumi za kila siku pasipo kuwa na wasiwasi wa gharama kubwa za matibabu pindi wanapopata matatizo ya kiafya” alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post