TAMWA YATOA MAFUNZO KWA WANAJAMII 66O KUPAMBANA NA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA UNGUJA


Baadhi ya wananchi wa shehia ya Bumbwini wilaya ya kaskazini B Unguja waliohudhuria katika mkutano maalumu wa utowaji wa elimu dhidi ya matendo ya udhalilishaji yaliotolewa na TAMWA-Zanzibar kwa kuhirikiana na Action Aid.
Wasanii kutoa taasisi ya Thesode wakionesha igizo ambalo linaashirikia kukamatwa na mhusika wa matukio ya udhalilishaji kwa wanawake huku lengo kuu likiwa ni kutoa elimu kwa jamii kutoyafumbia macho matendo hayo.

Na Muhammed Khamis,Tamwa-Zanzibar
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tamwa Zanzibar kwa kushirikiana na shirika la Action Aid kwa lengo la kupambana na udhalilishaji wa kijinsia wamewapatia mafunzo wanajamii 660 kutoka shehia 22 Wilaya ya Kaskazini B Unguja.

Afisa wa maswala ya udhalilishaji kutoka TAMWA-Zanzibar Zaina Salum Abdaala alisema lengo kuu la mafunzo hayo kwa wanajamii hususani wanawake ni kujengewa ufahamu zaidi juu ya dhana nzima ya udhalilishaji na madhara yake kwa kuwa bila ya kuwa na elimu sahihi dhidi ya matendo hayo hayataweza kumalizika.

Alieleza kuwa anaamini elimu hiyo ilitolewa kwa muda wa wiki mbili kwa wanajamii italeta mabadiliko makubwa ikiwemo wanajamii kufahamu viashiria vya udhalilishaji sambamba na umuhimu wa kutoa taarifa mara pale matukio hayo yanapojitokeza kwenye jamii.

Alisema kuwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar hadi sasa baadhi ya wanajamii wamekuwa wakiyafumbia macho matendo hayo kwa wanawake na watoto kutokana kuhofia sababu mbali mbali ikiwemo kuvunjika kwa ndoa zao.

"Kuna matukio mbali mbali ya udhalilishaji yanafanyika lakini watu wapo tayari kuona yanaendela lakini hushindwa kusema kwa kuhofia kupewa talaka na waume zao’’aliongeza.

Hata hivyo Afisa huyo aliasa jamii kubadilika na kutokuwa na muhali badala yake watoke na kutoa taarifa dhidi ya matendo hayo kwa lengo la kuchukuliwa hatua kali zaidi kwa watendaji wote watakaobainika kutenda unyama huo.

Akizungumza kwa niaba ya Masheha wenzake sheha wa shehia ya Kitope Khamis Ndende Juma alisema ni kweli kuwa wamekua wakikabiliwa na matukio mbali mbali ya udhalilishaji kwenye jamii zao kiasi cha kwamba walio wengi wameanza kushtuka na kuhofia madhara zaidi.

Alisema suala la muhali bado ni tatizo ambalo wanaendelea kukabiliana nalo ndani ya jamii zao kwa kuwa wapo baadhi ya watu wanatendewa matendo hayo na kisha kuamua kunyamaza kimya.

Hata hivyo Sheha huyo alisema kupitia elimu hio ilitolewa na TAMWA-Zanzibar anaamini kwa kiasi kikubwa itakwenda kubadili jamii na hatimae watu kuwa tayari kutoa ushirikiano wa kina dhidi ya matendo hayo kwa lengo la kuyamaliza kabisa.


Mzee Ali Makame kutoka shehia ya Kitope alisema ili jamii iweze kumaliza tatizo hilo ipo haja kuhakikisha wazazi na walezi wanakua karibu zaidi na watoto wao kila wakati.

Alisema baadhi ya matukio mengi yanayotokea yanaonesha wazi kuwa baadhi ya wazazi ama walenzi wamekosa umakini katika suala zima la uangalifu kwa watoto na wakati mwengine hua sababu ya kufanyiwa unyama huo.

Kwa upade wake Afisa Dawati la Jinsia Mkoa wa kaskazini Unguja Salum Khamis Machano alisema jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia wanajitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana na matukio hayo ikiwemo kuwachukulia hatua wale wote wanaofikishwa katika dawati hilo.

Hata hivyo Afisa huyo alisema bado kuna tatizo ndani ya jamii ikiwemo la kukosa utayari wa kuendelea na baadhi ya kesi ambazo huwa tayari zimeshafikishwa katika vituo mbalimbali vya polisi.

Aliomba jamii kubadilika na kuyachukuliwa matendo hayo kuwa ni ya kinyama na yasiopaswa kuvumiliwa kwa mtu yoyote yule awe mzee,mtoto ndugu au jirani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527