DC SINGIDA AWATAKA WAJASIRIAMALI KUWA NA NIDHAMU YA MATUMIZI YA FEDHA


Meneja wa SIDO mkoa wa Singida, Agnes Yesaya akitoa maelezo mafupi juu ya Mafunzo hayo
Mkufunzi wa somo la ukarabati na uimarishaji wa vyerehani, Dickson Shenkalwa akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida, Eng Paskasi Muragili juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili mafundi vyerehani
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Eng Paskasi Muragili akikabidhi Cheti cha kuhitimu Mafunzo ya Ujasiriamali kwa mmoja ya washiriki, Zainabu Saidi ambaye ni mlemavu wa viungo kwenye hafla ya ufungaji Mafunzo hayo.

Na Abby Nkungu, Singida
WAJASIRIAMALI wadogo mkoani Singida wametakiwa kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha wanazopata ili kuweza kukuza mitaji yao na kujiimarisha zaidi kiuchumi.

Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskasi Muragili wakati wa hafla fupi ya kufunga Mafunzo ya Wajasiriamali 68 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mjini Singida.

Alisema wajasiriamali wengi hupata vipato vya kutosha kupitia shughuli zao mbalimbali za kila siku lakini kutokana na kutokuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha hizo na kutojiwekea malengo, mara nyingi hujikuta hawana fedha kila wanapohitaji kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

"Huenda kinachochangia zaidi ni ukosefu wa elimu ya biashara kwa wajasiriamali hao hali inayosababisha washindwe kuweka kumbukumbu za mapato na matumizi ya fedha zao" alisema na kuongeza;

Mali bila daftari, hupotea bila habari. Huo ndio ukweli usiofichika. Ninyi mmepata bahati ya kufundishwa somo la Usimamizi wa biashara wakati wa mafunzo yenu hapa SIDO. Tumieni vyema ujuzi huo kwa kutunza kikamilifu mahesabu yenu ya kila siku ili kujitofautisha na wale ambao hawajapata elimu hiyo".

Awali, Meneja wa SIDO mkoa wa Singida Agnes Yesaya alieleza kuwa wahitimu hao walipata fursa ya kujifunza namna ya kukarabati vyerehani vyao na elimu ya awali ya biashara; hivyo akawataka waende kuwa chachu ya maendeleo kwenye maeneo yao ya kazi na kueneza habari njema za SIDO.

Naye mkufunzi wa somo la ukarabati na uimarishaji wa vyerehani, Dickson Shenkalwa alisema kuwa wengi wa washiriki wa mafunzo hayo hawakuwa na ujuzi wa kutosha juu ya zana wanazotumia.

"Wamekuwa wakiwaita mafundi ili kuwarekebishia hitilafu zinazojitokeza lakini kutokana na mafundi hao kutokuwa na ujuzi wa kutosha au kutaka kujipatia vipato vya kinyemela, matengenezo yanayofanyika huwa hayadumu. 

Wenye vyerehani huendelea kugharamia siku hadi siku huku wakichelewa kumaliza kazi za wateja wao.... Sasa, hawatakumbana na changamoto hizo tena", alisema. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527