ZAIDI YA WAKAZI 16,000 CHABULA KUPATA MAJISAFI NA SALAMA

Na Mohamed Saif-Magu

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema zaidi ya wakazi 16,000 kutoka Kata ya Chabula Wilayani Magu Mkoani Mwanza watanufaika na mradi wa maji wa Chabula-Bugando utakaotumia chanzo cha maji ya Ziwa Victoria.

Aweso amebainisha hayo Agosti 15, 2020 wakati wa ziara yake ya kukagua hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi huo utakaonufaisha wananchi kutoka vijiji vya Bugando, Chabula, Nyashigwe na Kongolo sambamba na kuzungumza na wataalam wanaoutekeleza.

Alibainisha kuwa ya lengo la Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maji ni kuwasogezea huduma ya majisafi na salama wananchi wake ili kuwaepushia usumbufu wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo muhimu.

“Azma ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli ni kumtua mwana mama ndoo kichwani kwa kumsogezea huduma ya maji ili kumuondolea kero iliyomsumbua kwa kipindi kirefu ya kutembea masafa marefu kutafuta maji,” alibainisha Naibu Waziri Aweso.

Aidha, alielekeza wataalam wanaotekeleza mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa hasa ikizingatiwa kwamba fedha ya utekelezaji wake inatoka kwa wakati.

Alibainisha kwamba Rais Magufuli ametoa zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwaajili ya kuhakikisha mradi wa Chabula-Bugando unakamilika haraka ili wananchi wapate maji na kwamba Wizara itahakikisha mradi unakamilika kwa wakati. 

"Tumesema sasa imetosha wananchi kuhangaika, hatuwezi tukawa na ziwa karibu hapa halafu wananchi walalamike hawana huduma ya majisafi; tunawahakikishia wananchi wote wa vijiji vya Bugando, Chabula, Nyashigwe na Kongolo kwamba mtapata majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria, huu ni mradi mkubwa na unatosheleza," alisema Naibu Waziri Aweso.

Vilevile alielekeza ajira zitokanazo na ujenzi wa mradi kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa wananchi wa eneo la mradi ili waanze kupata manufaa hata kabla ya mradi kukamilika kwa kujiongezea kipato.

Aweso aliwaasa wananchi wa maeneo yote ya mradi kuhakikisha wanautunza na kuulinda ili waendelee kunufaika kwa miaka mingi ijayo kama ulivyosanifiwa na hasa ikizingatiwa kwamba Serikali inatumia fedha nyingi kwenye ujenzi wake.

“Wananchi shirikianeni kuulinda na kuutunza huu mradi sambamba na kuhakikisha mnatunza chanzo cha maji ili uwe endelevu na muweze kunufaika nyinyi na vizazi vyenu,” alisema Aweso.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia mradi huo wa maji na alipongeza jitihada za Wizara ya Maji katika kuhakikisha miradi inajengwa kwa viwango na inakamilika kwa wakati.

Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa mradi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele alisema mradi unatekelezwa kwa ushirikiano wa wataalam wa ndani kutoka Wakala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na MWAUWASA.

Mhandisi Msenyele alisema mradi unajengwa kwa miezi tisa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.69 bila VAT ambazo zinahusisha ujenzi wa chanzo chenye uwezo wa kuzalisha lita za ujazo 75,000 kwa saa, ulazaji wa bomba kutoka ziwani, ujenzi wa tenki la lita 250,000 na ulazaji wa bomba za usambazaji.

Alibainisha kwamba tayari wamepokea kiasi cha shilingi milioni 550 kutoka Wizara ya Maji kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambao alisema ulianza kutekelezwa Aprili, 2020 na utakamilika Mwezi Desemba mwaka huu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post