Waziri Mkuu Atoa Agizo Kwa Wizara Ya Mifugo Na Uvuvi

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi ihakikishe inaboresha utoaji wa elimu ya ufugaji bora kwa wafugaji ili kuiwezesha mifugo yao kuwa na ubora na uzito mkubwa badala ya mifugo ya aina hiyo kuonekana kwenye maonesho pekee.

“Mara nyingi ng’ombe wenye uzito wa kilo mia nane, mia tisa nawakuta kwenye maonesho tu lakini hatuwaoni kwa wafugaji. Hawa anawatunza nani na kwa nini tusiwaambie wawatunze kama mnavyowatunza. Lazima tuwe na ng’ombe wanaofugwa na wafugaji wenye uzito huo, hivyo wafundisheni namna ya kuwatunza.”

Waziri Mkuu ambaye amemuwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika sherehe hizo ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Agosti 8, 2020) alipotembelea banda la Wizara hiyo katika kilele cha Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nane Nane Kitaifa kwenye Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu. Kauli mbiu ya sherehe hizo kwa mwaka huu ni “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020”.

“Nimetembelea baadhi ya mabanda kwenye viwanja hivi vya Nyakabindi na nimeona bidhaa nyingi zinazotokana na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, huu ni ushahidi tosha wa mchango wa sekta ya kilimo katika kufikia uchumi wa kati. Tukumbuke kwamba safari yetu ya kujenga uchumi wa viwanda inaendelea.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau mbalimbali walioitikia wito wa Serikali kwa kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata, kusindika na kutengeneza bidhaa zinazotokana na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Amesema kupitia maonesho hayo ya 28 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993, wakulima, wafugaji, wavuvi, wanaushirika na wajasiriamali hupata fursa ya kuonesha na kujifunza matumizi ya teknolojia bora za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji wa uhakika wa chakula sambamba na kukidhi mahitaji ya viwanda na masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Binafsi, nimefurahishwa na ubora wa bidhaa hizo, hakika mmejitahidi sana. Nimeridhika pasipo shaka kuwa wananchi waliotembelea viwanja hivi, nao wamepata fursa ya kujifunza na kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.”

Amesema kuwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ni malighafi muhimu kwenye viwanda na huchangia asilimia 65 ya malighafi zinazohitajika viwandani. Sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zimeendelea kutoa fursa nyingi za ajira kuliko sekta zote na asilimia 58 ya Watanzania wameajiriwa na kujiajiri katika sekta hizo.

Waziri Mkuu amesema kilimo ni mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa na katika  kipindi  cha  miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei za 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka sh. trilioni 25.2 mwaka 2015 hadi sh. trilioni 29.5 mwaka 2019.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewasihi wananchi wote washiriki kwenye mikutano ya kampeni ili kusikiliza sera za wagombea na kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kwa lengo la kuchagua viongozi bora kama kauli mbiu ya Nanenane mwaka huu inavyosema.
      
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itahakikisha kuwa wananchi wote wanaendelea kuwa salama kwa kusimamia kikamilifu amani, utulivu, umoja, undugu na ushirikiano wa Watanzania uliojengwa tangu kuanzishwa kwa Taifa letu.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanasiasa wote nchini wakati wa kufanya kampeni utakapofika wafanye kampeni za kistaarabu wa waepuke matumizi ya lugha za uchochezi ambazo zinaweza kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu.

“Sote tunafahamu kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu. Sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji ni miongoni mwa sekta za uzalishaji ambazo maendeleo yake yanategemea kwa kiasi kikubwa uongozi bora. Nchi yetu inahitaji viongozi watakaokuwa chachu ya kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuinua ustawi wa maisha ya wakulima, wafugaji na wavuvi.”

Waziri Mkuu amesema viongozi bora ni muhimu katika kuhakikisha uwekezaji kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa na tija, unazingatia matumizi ya teknolojia za kisasa na kuongeza thamani ya mazao kwa kuzalisha bidhaa kupitia viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments