WAZIRI MKUU APONGEZA UJENZI WA MRADI WA KUONGEZA UWEZO WA KUHIFADHI NAFAKA UNAOTEKELEZWA NA NFRA


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa amepongeza ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa Mradi unaotekelezwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo jana tarehe 8 Agosti 2020 wakati alipotembelea Banda la NFRA kabla ya kuhitimisha maadhimisho ya sherehe za wakulima Nanenane katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Waziri Mkuu amesema kuwa ujenzi huo ni mahususi kwa ajili ya Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Nafaka kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000.

Akitoa taarifa ya Mradi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA Ndg Milton Lupa amesema Mradi huo unajumuisha ujenzi wa vihenge 56 na maghala ya kisasa 9 ambavyo kwa pamoja vinaongeza uwezo wa kuhifadhi kwa tani 250,000. Kwa sasa Mradi huu umefikia umefikia asilimia 75 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2020/2021.

Amesema Uhifadhi wa nafaka kwa kutumia maghala ya kawaida, akiba inaweza kuhifadhiwa kwa takriban miaka mitatu tu kabla ya kuanza kupoteza ubora. Kwa kutumia vihenge vya kisasa, akiba inaweza kuhifadhiwa hata kwa zaidi ya miaka mitano bila kupoteza kiwango cha ubora

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ni Taasisi ya Umma chini ya Wizara ya Kilimo iliyoanzishwa chini ya Sheria za Wakala wa Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 na kuanza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2008.

NFRA ina jukumu kuu la kuhakikisha usalama wa chakula ndani ya nchi kwa kununua, kuhifadhi na kutoa chakula katika maeneo yenye upungufu na kwa waathirika wa majanga mbalimbali.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post