WAZIRI JAFO AITAKA TARI KUTOA ELIMU YA ZAO LA ZABIBU SHULENI

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) katika kituo cha Makutupora kuhakikisha inakuwa na mkakati wa Kutoa elimu ya Zao la zabibu katika shule zinazozungukwa na zao hilo hususan Dodoma.


Waziri Jafo ameyasema hayo  Agosti 3,2020  katika Viwanja vya Nanenane jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 27 ya sherehe  hizo Kanda ya Kati.

Waziri Jafo amesema kutokana na kuwa na aina mbalimbali ya zao la zabibu na matumizi kuwa tofauti hivyo ni vyema elimu hiyo ikatolewa katika shule mbalimbali  ili vijana wakawa na uwezo mzuri wa kutoa elimu katika jamii aina ya zabibu na matumizi yake  huku akizitaka Halmashauri zote nchini kutoa elimu ya kilimo na Ufugaji kwa wananchi ili sekta hizo zilete tija kwa jamii na taifa.

Pia amewataka watafiti wa sekta mbalimbali kuutumia utafiti wao kwa kuisaidia Serikali kuinua  sekta ya Kilimo,Ufugani na Uvuvi kwa kutembelea wanaojishughulisha na shughuli hizo kuwajengea uwezo.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amebainisha kuwa  ipo haja ya kuanzishwa maonesho ya Nanenane ngazi ya  Kaya ili kuwapatia wananchi  mbinu bora na ubunifu katika  kwendana na soko huku Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt..Binilith Mahenge akiwahimiza wakazi wa Dodoma kujitokeza na kutembelea mabanda kuongeza ubunifu na kuwa mabalozi katika maeneo yao.

Naye Mkurugenzi wa  Kampuni ya Mkulima Smart Bw.Honoratus  Salvatory amebainisha kuwa katika mradi wake wa kuzalisha mkojo wa Sungura umekuwa na tija kubwa kwani mkojo huo ni moja ya mbolea muhimu katika ustawishaji  wa mimea ya mazao mbalimbali huku akiwaasa wananchi kutembelea  maonesho ya nanenane  kama sehemu ya kujifunza na kufanyia kazi na si kutalii pekee.

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527