TANZANIA YASAINI MKATABA WA MAPITIO WA GEORGETOWN WA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, CARIBBEAN NA PACIFIC


Tanzania imesaini Mkataba wa mapitio wa Georgetown unaosimamia  mahusiano na uendeshaji wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribiani na Pasifiki ambayo zamani ilikuwa ikiitwa  ACP na sasa Organisation of African, Carribean and Pacific States (OACPS) iliyo na nchi wanachama 79.

Mkataba huo ulisainiwa na balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji,  Mhe. Jestas Abuok Nyamanga kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Brussels, Ubelgiji tarehe 31 Julai 2020. Hivyo Tanzania inakuwa nchi ya 42 kati ya nchi 79 kusaini Mkataba wa mapitio wa Georgetown.

Mkataba wa Georgetown umefanyiwa mapitio ili uweze kuendana na wakati kwa kuzingatia mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea duniani katika nyanja za  kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimazingira tangu kuanzishwa kwa ACP mwaka 1975. Mchakato wa kufanya mapitio ya mkataba huu ulianza mwezi Machi 2013 kupitia timu maalum iliyoanzishwa kukusanya maoni na kuleta mapendekezo chini ya Uenyekiti wa Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Olusegun Obasanjo.

Aidha, Mwaka 2019 mchakato wa mapitio hayo ulihitimishwa kwa  kuridhiwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za OACPS katika mkutano wao uliofanyika mwezi Desemba 2019 jijini Nairobi, Kenya.

Mkataba wa Georgetown ndiyo ulianzisha ACP mwaka 1975 katika mji wa Georgetown nchini Guyana.  Tanzania ilisaini Mkataba huo wa awali tarehe 11 Desemba 1975 na imedumu ikiwa mwanachama wa ACP tangu wakati huo.

Pamoja na kuwa mwanachama Tanzania imekuwa ikinufaika katika masuala ya kiuchumi, kijamii, biashara, na uwekezaji kupitia ushirikiano maalum baina ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya unaosimamiwa na mikataba ya Lome na Cotonou. Vilevile miradi ya ubia wa maendeleo na ile ya mtangamano wa nchi za ACP chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya. Pia ushirikiano katika masuala ya kubadilishana ujuzi na uzoefu na nchi za ACP, mshikamano wa kisiasa na kidiplomasia katika kutetea maslahi ya Tanzania kimataifa kupitia jukwaa la ACP.

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post