Biden amteua mwanamke wa kwanza mweusi Kamala Harris kuwa mgombea mwenza Urais Marekani

Mgombea urais kupitia chama cha Democratic nchini Marekani Joe Biden, amemteua Seneta wa California Kamala Harris, kuwa mgombea mwenza wakati wa uchaguzi wa urais utakaofanyika mwezi Novemba.

Uteuzi wa Bi Harris, unamaliza subira ya miezi kadhaa kufahamu ni nani atakuwa mgombea mwenza wa Biden, ambaye atapambana na rais Donald Trump.

Harris ambaye pia aliwahi kutia nia ya kutaka kuwa mgombea urais, iwapo chama cha Democratic kitashinda, anatarajiwa kuwa makamu wa rais wa kwanza Mwanamke mweusi mwenye asili ya India.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa Harris mwenye umri wa miaka 55 ambaye ana historia ya kubaguliwa kwa sababu ya rangi yake na kuwa mpambanaji, anatarajiwa kuvutia wapigakura wanaohisi kutothaminiwa nchini Marekani.

Katika historia ya siasa nchini Marekani, Bi Harris anakuwa mgombea wa tatu mwanamke, akitanguliwa na Geraldine Ferraro mwaka 1984 na Sarah Palin mwaka 2008.

Harris amesema ameheshimika sana kuteuliwa kama mgombea mwenza na atafanya kila analoweza kumsaidia, Biden kushinda Uchaguzi huo na kumwelezea kama kiongozi aliye na uwezo wa kuwaunganisha Wamarekani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post