BAKITA YATOA ELIMU KWA BAADHI YA MANENO YA KISWAHILI YANAYOPOTOSHWA

Na. Anitha Jonas – WHUSM, DODOMA

Baadhi ya watanzania wamekuwa na hulka ya kutokuwa na matumizi sahihi ya baadhi ya maneno ya lugha ya Kiswahili, hali ambayo imesababisha Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ikiwa ni  taasisi yenye dhamana kuanza kutoa elimu sahihi yamatumizi ya  maneno ya lugha hiyo.


Kaimu Katibu Mtendaji wa BAKITA Bibi. Consolata Mushi, hivi karibuni alipokuwa akizungumza kwa njia ya simu na Afisa Habari wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Bibi. Anitha Jonas alisema kuwa baadhi ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili wamekuwa wakifanya makosa ya matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Aidha, Bi.Consolata alisema kuwa baadhi ya maneno yamekuwa yakitumiwa kimakosa na utumiaji huo umepelekea kuibua mgogoro wa kifikra miongoni mwa watumiaji wa lugha husika hivyo kuepukana na madhara yanayoweza kuwa makubwa ni bora kusahihisha matumizi hayo.

“Nitoe mfano ambao ulisikika siku moja kupitia chombo fulani cha habari kuwa mtaalamu wa kilimo amewaasa wakulima kutumia mbolea, utumiaji wa namna hii si tu kwamba unapotosha bali unaharibu kabisa dhana nzima ya kile kinachosemwa,”alisema Bibi.Consolata

 Akitolea mfano wa maneno ambayo yanapotoshwa ni neno ‘asa’ kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili (2015) lina maana ya “Kanya au kataza mtu kufanya jambo fulani”, na  kusema kuwa matumizi hayo yanaweza kupotosha na kuharibu maana ujumbe uliokusudiwa.

Vilevile, Bibi.Consolata alifafanua matumizi sahihi ya neno ‘asa’ kuwa linaweza kutumika kwa kuonya mfano: “Walimu wamewaasa wanafunzi kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya” au “Serikali yawaasa wazazi wanaowaachisha watoto wao shule kwa ajili ya kuwaoza.

Kwa mujibu wa BAKITA neno lingine ambalo limekuwa likipotoshwa  na watumiaji wa lugha ya Kiswahili ni mrabaha, chanzo cha upotoshaji wa neno hilo ni ubadilishaji wa mpangilio wa vitamkwa vya mwisho vinavyounda neno hilo, badala ya kusema mrabaha watu husema  mrahaba.

Mrabaha maana yake ni, “Malipo yanayotolewa na mchapishaji kwa mtunzi wa kitabu kwa kipindi fulani kama sehemu ya mauzo ya kitabu kinachohusika, au  inaweza kuwa ni “Malipo yanayotolewa kama sehemu ya faida inayotokana na biashara fulani.

Halikadhalika, neno mrahaba halina maana yoyote katika lugha ya Kiswahili hivyo utumiaji wa neno hilo ni upotoshaji na watu wengi wamekuwa wakifanya makosa katika matumizi yake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post