PROF. MDOE ARIDHISHWA NA MAANDALIZI NA UONGOZI WA SUA KWAAJILI YA KUWAPOKEA WANAFUNZI


Picha ya pamoja ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda(kulia) Naibu katibu Mkuu Prof. James Mdoe( wa pili kutoka kulia) Mkuu wa Kampasi ya Mizengo Pinda Prof. George Mwamengele( wa kwanza kushoto na Msaidizi wake upande wa Taaluma Prof. Sikira( wa pili kutoka kushoto).
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na teknolojia Prof. James Mdoe akizungumza na viongozi na watumishi wa SUA Kwenye Kampasi hiyo mara baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea majengo ya Kampasi hiyo.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda aki(wa kwanza kushoto) akiongea akitoa maelezo mafupi juu ya Kampasi hiyo ilipotoka na ilipo sasa, kushoto kwake ni Msaidizi wa Mkuu wa Kampasi hiyo upande wa Taaluma Prof. Sikira.
Naibu Katibu Mkuu Prof. Mdoe akionyeshwa shamba kubwa ambalo pia limetolewa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda kwaajili ya Kampasi hiyo.
Prof. Sikira ambaye ni msaidizi wa Mkuu wa kampasi hiyo kwenye masuala ya Taaluma akimuonyesha Prof. Mdoe moja kati ya viti na meza za awali zilizokuwa zimewekwa wakati huyo kabla ya kukabidhiwa kwa SUA.
Mkuu wa Kampasi ya Mizengo Pinda Prof. George Mwamengele akimuonyesha Naibu katibu Mkuu huyo Prof. James Mdoe moja ya madarasa yakiwa tayari kwaajili ya Wanafunzi kusoma.
Mkuu wa Kampasi ya SUA - Mizengo Pinda Mkoani Katavi Prof. George Mwamengele akitoa maelezo ya maandalizi ya kupokea wanafunzi kwa Mwaka huu wa masomo.
Prof. Raphael Chibunda ( wa pili kulia) akimuongoza Naibu Katibu Mkuu kutembelea majengo ya Kampasi hiyo.
Prof. Chibunda akimuonesha Prof. Mdoe moja ya vyumba ambavyo vinatumika kama sehemu za kulala wanafunzi vikubwa tayari kuwekwa magodoro tu.

**********************************

Na: Calvin Gwabara – KATAVI

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu sayansi na teknolojia Prof. James Mdoe ameridhishwa na maandalizi yaliyofanywa na Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwaajili ya kuwapokea wanafunzi na kuanza rasmi kwa Kampasi ya Mizengo Pinda Mkoani Katavi.

Prof. Mdoe ameyasema hayo wakati alipotembelea kampasi hiyo mpya ya SUA iliyopewa jina la Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda alipokwenda kujionea maandalizi na mazingira ya kampasi hiyo ambayo unatarajia kupokea wanafunzi tarehe 23/11/2020.

Naibu katibu Mkuu huyo amesema uanzishwaji wa kampasi hiyo unasaidia jitihada za Serikali kupitia Wizara yake kwenye kuongeza nafasi nyingi zaidi za wanafunzi wenye sifa na wanaotaka kusoma elimu ya juu hasa baada ya maboresho makubwa ya elimu yanayofanywa na Serikali nchi nzima kwenye elimu ya Msingi na sekondari.

“ Kwanza niwapongeze sana SUA na uongozi mzima kwa kazi kubwa ambayo mmeshaifanya ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya kampasi hii, na sisi Kama Wizara tunawaahidi kuwasaidia ujenzi wa Bweni kubwa haraka ili Mwaka ujao wa masomo iwe imekamilika na itumike kuwezesha wanafunzi kuishi vizuri maana najua watakuwa wengi Mwaka ujao” Alisema Prof. Mdoe.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwashauri SUA kuanzisha kozi fupifupi zitakazoweza kusaidia kuleta ujuzi kwa wananchi wa eneo hilo na Mkoa kwa ujumla ambazo hazihitaji mtu kuwa na sifa bali kutoa ujuzi kulingana na mahitaji ya wananchi hasa wale ambao hata hawajafika kidato cha nne.

Naibu katibu Mkuu huyo awepongeza uzalendo Mkubwa aliouonyesha Waziri Mkuu mstaafu Mhe. Mizengo Pinda kwa kuyatoa majengo hayo na Ardhi Kama shamba kwaajili ya kuanzisha kampasi hiyo na kuitaka jamii kuiga mfano huo wa aina yake kwa manufaa ya Umma.

Akitoa taarifa fupi ya kampasi hiyo ya Mizengo Pinda Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda ameishukuru Serikali kwa jitihada kubwa ambazo inazifanya katika kuboresha was mazingira ya kufundishia kuanzia Shule za msingi hadi vyuo vikuu na hivyo kuwezesha Watanzania wengi zaidi kupata elimu.

Prof. Chibunda amesema mara baada ya kukabidhiwa majengo hayo na Waziri Mkuu huyo Mstaafu Mhe. Pinda waliofanya tathimini na kutenga kiasi cha shilingi milioni 200 kwaajili ya ukarabati lakini hadi kufikia hapa tayari wamesharumia kiasi cha shilingi milioni 810 na bado kazi inaendelea ili kuwezesha wanafunzi watakapoingia mazingira yote yawe tayari.

Ameongeza kuwa Mtendaji Mkuu wa Tume ya vyuo vikuu alipata nafasi ya kunitembelea Kampasi hiyo yeye mwenyewe na anashukuru kuwa sasa wamepata ithibati ya kuanza kupokea wanafunzi kwa Mwaka huu kwa Kozi tatu maalumu kulingana na mahitaji ya Mkoa wa Katavi na mikoa mingine jirani.

“ Maono yetu kama Chuo ni kuona ukaenda huu unakuwa na Chuo kikubwa na hivyo kuchochea Elimu na ujuzi kwa Wananchi badala ya wahitimu kwenda mbali kama Morogoro na Dar es salama kusoma vyuo vikuu, hapa ni mahali sahihi sana kwa kutolea elimu pengine tofauti na maeneo mengine hivyo ni matumaini yetu kuwa vijana wa maeneo haya watakuwa wengi kuliko mikoa mengine” Alisema Prof. Chibunda.

Akizungumzia Kozi zitakazoanza kutolewa hapo Mkuu wa Kampasi hiyo Prof. George Mwamengele amesema wataanza na kozi tatu ambapo moja ni Astashahada ya Uongizaji watalii na Uwindaji salama, kozi ya pili ni Stashahada ya Kilimo na kozi ya tatu ni Shahada ya Nyuki na Mazao yatokanayo na Nyuki.

Prof. Mwamengele amesema maandalizi kwa kiasi kikubwa yamekamilika kwa maana ya miundombinu kama vile madarasa, Mabweni, Mifumo ya Mtandao lakini pia Chuo kimeajiri walimu wapya wa kutosha na wengine wakongwe wamehakishiwa kampasi hiyo kutoka SUA kampasi kuu Mkoani Morogoro.

Dirisha la maombi kwa wanafunzi wa kozi mbalimbali kwenye kampasi kuu na kampasi hii mpya ya Mizengo Pinda litakuwa wazi kuanzia tarehe 31/08/2020 na Wanafunzi kwa mujibu wa kalenda ya masomo wanatakiwa kuwasili Chuo kwaajili ya kuanza masomo tarehe 23/11/2020.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527