DC JOKATE MWEGELO ATIMIZA AHADI KWA AKINA MAMA KISARAWE


Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Jokate Mwegelo akiwa na kikundi cha akina Mama wa Raha Tupu cha Masaki, Kisarawe mwanzoni mwa mwaka huu.
Muonekano wa jengo hilo la kisasa ambalo limekamilika kwa asilimia 90.
Na Andrew Chale - Kisarawe
Mkuu  wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Jokate Mwegelo amesema wamejipanga kuhakikisha wananchi wanafikiwa na maendeleo ikiwemo kuchangamkia fursa zilizopo katika Wilaya hiyo ikiwemo za Utalii, Kilimo na uwekezaji.

Jokate amesema hayo kufuatia kukamilika kwa jengo jipya na la kisasa la kutolea huduma za Chakula la kikundi cha akina mama cha Raha Tupu wa kijiji cha Masaki ambapo aliahidi na kutimiza.

"Mwanzoni mwa mwaka huu nilitembelea kikundi cha akina mama cha Raha Tupu wa Kijiji cha Masaki mazingira ya sehemu wanatolea huduma ya chakula ilikuwa ndani ya banda la makuti. 

Mwezi uliopita tulipata fedha na kuanza ujenzi wa jengo la kisasa na ndani ya wiki tatu tumeweza kujenga jengo hilo jipya kama mnavyoona (Pichani)",alisema DC Jokate.

Aidha, aliwapongeza wadau kwa kumuunga mkono mpaka kufanikisha ujenzi huo ambao anaamini utakuwa chachu kwa akina mama hao.

"Niwashukuru Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa mchango wao na Halmashauri ya Wilaya Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa usimamizi mzuri mpaka sasa. 

Lakini pia kampuni ya Coca-Cola. Kuna mambo mazuri tutafanya zaidi hapa kijiji cha Masaki" ,alisema Jokate.

Jokate pia alimshukuru, Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kupeleka maendeleo kwa wananchi wa Wilaya hiyo.

"Baada ya Mhe Rais kufanya ziara Kisarawe na kuelekeza barabara kukarabatiwa kwa kiwango cha lami kutoka Kisarawe mpaka Vikumburu kuelekea Hifadhi mpya ya Taifa ya Mwalimu Nyerere.

Sisi viongozi hatujalaza damu. Tumeanza kutengeneza fursa kwa wananchi hasa za maeneo ya Watalii ikiwa ni pamoja na kupata chakula cha Asili na jengo ili la kisasa ni kielelezo", alimalizia Jokate.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527