WAZIRI KAIRUKI AIPONGEZA BENKI YA CRDB UWEZESHAJI PEMBEJEO ZA KILIMO



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki akimkabidhi trekta mkulima Raphael Kasawa ambaye ni mteja wa Benki ya CRDB lenye thamani ya shilingi milioni 65.5 huku akishuhudiwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga

Simiyu - Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kusaidia kuboresha kilimo nchini kwa kuwawezesha wakulima kupata pembejeo za kisasa zinazosaidia kuongeza tija ya kilimo chao. Kairuki alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi trekta kwa mkulima wa mahindi Raphael James wakati wa maonesho ya Nanenane yanayoendelea kitaifa mkoani Simiyu. 
Akikabidhi trekta hilo lenye thamani ya shilingi milioni 65.5,Waziri Kairuki amesema ili kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini wakulima wanapaswa kuwekeza katika pembejeo za kisasa na kuacha kutegemea kilimo cha jembe la mkono. “Niipongeze sana Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele kuwawezesha wakulima, kama taifa tukiwekeza vya kutosha katika kilimo sio tu tutasaidia wakulima wetu kujiongezea kipato bali pia tutaongeza malighafi katika viwanada vyetu na hivyo kuzidi kuchochea uwekezaji katika sekta ya viwanda,” aliongezea Waziri Kairuki huku akizitaka taaisisi nyengine za fedha kuiga mfano wa Benki ya CRDB.
Meneja Mwandamizi wa Kilimo Biashara, Maregesi Shaban akitoa maelezo kwa Waziri Kairuki namna ya Benki ya CRDB inavyofanya uwezeshaji huo wa pembejeo kwa wakulima akishuhudia katikati ni Waziri wa kilimo, Japhet Hasunga.

Akitoa maelezo kwa Waziri Kairuki namna ya Benki ya CRDB inavyofanya uwezeshaji huo wa pembejeo kwa wakulima, Meneja Mwandamizi wa Kilimo Biashara, Maregesi Shaban alisema Benki ya CRDB kwa kushirikiana na kampuni ya ETC Agro imekuwa ikitoa mikopo nafuu ya matrekta ya Mahindra kwa wakulima ambapo Benki inatoa asilimia 65 ya gharama za trekta huku mteja akichangia asilimia 35 ya gharama.

“Mkopo ni wa masharti nafuu sana na riba yake ni nafuu, lakini pia mkulima haitaji dhamana ili kupata mkopo huu, dhamana ni trekta lenyewe,” alisema Maregesi huku akibainisha kuwa mbali na unafuu wa kupata mkopo huo mkulima pia atakuwa akipata usaidizi wa namna ya kuhudumia trekta na matengenezo baada ya manunuzi kutoka kwa wataalamu wa ETC Agro.

“Tupo hapa Nanenane lakini mkulima anaweza kupata mkopo huu kwa kutembelea matawi yetu yaliyopo nchi nzima,” alisema Maregesi.

IMG_8957 (1)
Mteja wa Benki ya CRDB, Raphael Kasawa akimwelezea Mheshimiwa Waziri, Angellah Kairuki namna alivyoona fursa mara baada ya kutembelea katika banda la Benki hiyo na kupata maelezo ya kuwezeshwa mikopo yenye unafuu katika kukopeshwa Pembejeo za kilimo na kuamua kuchangamkia mara moja.


Kwa upande wake mkulima Raphael Kasawa, aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mkombozi wa wakulima wadogo kama yeye, huku akiwahamasisha wakulima wengine kujitokeza kuchangamkia fursa hizo za uwezeshaji wakulima zinazotolewa na Benki ya CRDB.

“Mwanzoni nilikuwa nikilima heka chache kwa tabu huku nikitegemea trekta la kukodi, lakini sasa hivi nitaweza kulima heka nyingi zaidi zaidi ya heka miamoja, kwani ninatarajia kuwa na shamba jengine lenye zaidi ya heka 50,” alisema Kasawa huku akibainisha kuwa trekta hilo pia atalitumia kuwasaidia wakulima wenzake.

Mpaka sasa Benki ya CRDB imeshakopesha zaidi ya TZS. 650 Billioni kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Mikopo itolewayo na Benki ya CRDB kwenye sekta ya kilimo ni sawa na asilimia 40 ya mikopo yote itolewayo na mabenki yote kwenye sekta hii muhimu kwa maendeleo ya taifa. 
C:\Users\User\Desktop\Picha Nane Nane\IMG_8934 (2).JPG

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527