CCM KUZINDUA RASMI KAMPENI ZAKE KESHO AGOSTI 29 JIJINI DODOMA


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)kimesema kesho Agosti 29 mwaka huu wa 2020 wana jambo lao ambalo ni la uzinduzi rasmi wa Kampeni za Mgombea wa Urais wa Chama hicho Dk.John Magufuli huku kikieleza kitatumia nafasi hiyo kuielezea Afrika na Dunia mambo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ga Tano.

Akizungumza leo Agosti 28,2020, katika Uwanja Jamhuri jijini Dodoma ,Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Humphrey Polepole amefafanua maandalizi yote kuelekea uzinduzi wa kampeni za mgombea Urais na ratiba itaanza saa moja asubuhi hadi saa 12 jioni.

"Watanzania na wana CCM kesho hapa uwanja wa Jamhuri tuna jambo letu tunawakaribisha wote.Kesho tunataka kuisimamisha Tanzania,Afrika na Dunia kwa kuelezea mafanikio ambayo yamepatika katika kipindi cha miaka mitano chini ya jemedari wetu Dk.John Magufuli,"amesema Polepole na kusisitiza watu watafurika uwanjani hapo kuanzia saa 12 asubuhi.
.
Amesema kwamba baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) kutangaza kwamba kampeni za Uchaguzi Mkuu zitaanza Agosti 26, mwaka huu , CCM iliamua kujipa siku tatu za kuweka mambo sawa na kesho ndio siku ambayo kazi inaanza ya kumuombea kura mgonbea urais wa Chama hicho.

Polepole ameeleza kwamba katika siku ya kesho ambayo ni maalum ya kuzindua kampeni za mgonbea urais wa CCM pamoja na mambo mengine itakuwa siku ya kueleza mambo makubwa yaliyofanywa na Serikali.

Na kwamba kutakuwa na orodha ndefu ya Watanzania ambao wamejaaliwa kutumia lugha rahisi na nyepesi kuelezea mambo ambayo yamefanywa na Serikali katika kipindi cha miaka mitano ambayo kimsingi yameifanya nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo ambayo kila mmoja wetu ni shahidi.

Hata hivyo amesema licha ya ratiba kuanza asubuhi sambamba na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, itakapofika saa saba mchana ndio utakuwa muda maalum wa kuanza kuelezea mambo makubwa yaliyofanyika nchini.

Polepole ambaye kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari alikagua shughuli za maandalizi, amesema mbali ya kuelezea mafanikio,pia Mgombea wao Dk.Magufuli ataelezea maono ya mambo makubwa ambayo atayafanya katika miaka mitano ijayo.

"Tunataka kuwaonesha Watanzania namna ambavyo miaka mitano imekuwa ya mafanikio makubwa,miaka mitano ya kumshukuru Mungu na miaka mitano ya kueleze yale ambayo yanakwenda kufanyika.Kesho tutakuwa mubashara katika vyombo mbalimbali vya habari na kwa hapa uwanjani tumejipanga vizuri kwani kutakuwa na maelfu ya wananchi ndani ya uwanja na nje ya uwanja ambako tumeweka skrini kubwa kuonesha matukio yote yatakayokuwa yanaendelea.

Wakati maandalizi yakiwa yamekamilika katika uwanja wa Jamhuri, wakazi wq Jiji la Dodoma ambao wamezungumza na Michuzi TV na Michuzi Blog wameeleza kuwa wanasubiri kwa hamu uzinduzi huo wa kampeni za mgombea urais wa CCM na kimsingi kesho mapema watakuwa wamefika uwanjani kushuhudia tukio hilo la kihistoria hasa kwa kutambua kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527