VIONGOZI MBALIMBALI KUTOKA NJE YA TANZANIA WAANZA KUWASILI NCHINI KUHUDHURIA MAZISHI YA RAIS MSTAAFU BENJAMIN WILLIAM MKAPA


Viongozi mbalimbali kutoka nje ya Tanzania wameanza kuwasili nchini kuhudhuria maziko ya kitaifa ya Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Benjamin William Mkapa aliyefariki usiku wa kuamkia ijumaa ya Julai 24,2020 Jijini Dar es Salaam.


Waziri Mkuu wa Burundi Jenerali Alain Guillaume Bunyoni amekuwa kiongozi wa kwanza kutoka mataifa ya nje kuwasili hapa nchini majira ya saa tano na dakika 20 kwa ndege ya Shirika la ndege la (Tanzania Air Tanzania) ambapo amesema Burundi imepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha Hayati Benjamin William Mkapa na hivyo kutokana na urafiki wa kindugu baina ya Tanzania na Burundi amekuja nchini kuwakilisha wananchi Waburundi kuomboleza na Watanzania kifo cha Mkapa.

Katika msafara wake Waziri Mkuu huyo ameambatana pia na Spika wa Baraza la Seneti la Burundi Mhe. Reverien Ndikuriyo ambaye kwa upande wake amesema kifo kimeyapokonya Maisha ya Hayati Benjamin William Mkapa ambaye bado alikuwa akihitajika kwa kiasi kikubwa hususani na Bara la Afrika kutokana na uwezo wake mkubwa aliokuwa nao katika usuluhishi na hivyo Burundi imempoteza msuluhishi mkubwa.

Mbali na Spika wa Baraza la Seneti la Burundi Mhe. Reverien Ndikuriyo,pia Waziri Mkuu wa Burundi Jenerali Alain Guillaume Bunyoni ameambatana na Naibu katibu Mkuu wa chama kinachotawala nchini Burundi cha CNDD-FDD Mhe. Joseph Ntakarutimana.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea viongozi hao Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema wageni hao wamewasili jana Mkoani Kigoma wakitokea Burundi na baadae kupanda ndege na kuwasili Dar es Salaam hii leo na kuongeza kuwa ujio wa viongozi hao wa Burundi unaidhihirishia dunia mahusiano mema nay a kindugu yaliyopo kati ya Tanzania na Burundi bila ya kujali nyakati za shida,kuomboleza ama raha.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kutoa taarifa za kuwasili kwa viongozi wa Mataifa mbalimbali katika maziko ya kitaifa ya Hayati Benjamin William Mkapa kwa kadri zitakavyopokelewa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527