SIMBA SC WAKABIDHIWA KOMBE LA 21 LIGI KUU


Mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo, Simba SC leo wamelazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji, Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Sare hiyo ya tatu mfululizo na ya bila mabao, inaifanya Simba SC ifikishe pointi 81 baada ya kucheza mechi 34 na sasa inawazidi pointi 19 Azam FC na 20 Yanga SC wanaofuatia nafasi ya pili na ya tatu. 

Baada ya mchezo huo uliochezeshwa na refa Hamdani Said wa Mtwara aliyesaidiwa na Credo Mbuya wa Mbeya na Abdallah Lisakasa wa Lindi, kikosi cha Simba SC kimekabidhiwa Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu ambalo litakuwa la kwao moja kwa moja kutokana na kulitwaa mara tatu mfululizo. 

Hilo linakuwa taji la 21 la Ligi Kuu kwa Simba SC baada ya awali kubeba taji hilo katika misimu ya 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2010, 2012, 2018 na 2019.

Vigogo, Yanga SC wanabaki kuwa mabingwa mara nyingi zaidi wa taji hilo, 26 katika misimu ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011, 2013, 2015, 2016 na 2017.

Timu nyingine zilizobeba taji hilo ni Cosmopolitans ya Dar es Salaam 1967, Mseto SC ya Morogoro 1975, Pan African ya Dar es Salaam 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986, Coastal Union ya Tanga 1988, Mtibwa Sugar ya Morogoro 1999 na 2000 na Azam FC 2014.

Kikosi cha Namungo kilikuwa; Nourdine Balora, Miza Christom, Edward Manyama, Stephen Duah, Carlos Protas, Hamisi Khalifa, Hashim Manyanya/Jamal Issa dk73, Steve Nzigamasabo, Bigirimana Blaise/John Kelvin dk31, Lucas Kikoti na Abeid Athumani.

Simba SC; Beno Kakolanya, Haruna Shamte/Hassan Dilunga dk63, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili, Tairone Santos/Gardiel Michael dk52, Said Hamisi, Miraji Athumani ‘Madenge’, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/Cyprian Kipenye dk71 na Francis Kahata/Deo Kanda dk63.

 CHANZO- BINZUBEIRY BLOG

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527