SIMBA SC YAICHAPA AZAM FC 2-0 ...KUKUTANA NA YANGA NUSU FAINALI KOMBE LA TFF


WATANI wa jadi, Simba na Yanga SC watakutana katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup baadaye mwezi huu.

Hiyo ni baada ya Wekundu wa Msimbazi kufanikiwa kuitoa Azam FC kwa kuichapa mabao 2-0 katika mchezo wa mwisho wa Robo Fainali usiku wa leo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Mbali na Simba SC kumenyana na Yanga SC walioitoa Kagera Sugar ya Bukoba jana kwa kuwachapa 2-1 jana Uwanja wa Taifa pia - Sahare All Stars itamenyana na Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi iliyoitoa Alliance FC ya Mwanza jana kwa kuichapa 2-0.

Nahodha John Raphael Bocco aliifungia Azam FC bao la kwanza dakika ya 39 kwa kichwa akimalizia krosi nzuri ya kiungo Mkenya, Francis Kahata Nyambura kutokamupande wa kushoto.
Clatous Chota Chama akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 56 akimalizia pasi ya beki Shomari Salum Kapombe kutoka upande wa kulia.

Mechi ya kwanza Sahare All Stars ya Daraja la Kwanza ilifanikiwa kwenda Nusu Fainali baada ya kuichapa Ndanda SC ya Mtwara kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.

Katika dakika 90 za mchezo, Kassim Haruna alianza kuifungia Sahare All Stars dakika ya 49 kabla ya Abdul Khamis kuisawazishia Ndanda SC kwa penalti dakika ya 54.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’/Gardiel Michael dk88, Kennedy Juma/Erasto Nyoni dk46, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Gerson Fraga ‘Viera’, Clatous Chama, John Bocco, Luis Miquissone na Francs Kahata.

Azam FC; Benedict Haule, Nico Wadada, Salmin Hoza, Oscar Maasai, Abdallah Kheri, Mudathir Yahya/Bryson Raphael dk46, Bruce Kangwa/Iddi Kipagwile dk68, Frank Domayo, Richard Ella D’jodi, Never Tegere/Andrew Simchimba dk64 na Obrey Chirwa/Shaaban Iddi Chilunda dk76.

 Chanzo - Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527