NDUGU WAFUKUA MAITI ILIYOZIKWA MIEZI 3 JIJINI MBEYA


Ndugu wa Marehemu Tulizo Konga wa Kijiji cha Igumbilo Kata ya Chimala mkoani Mbeya, wamefukua kaburi la ndugu yao mara baada ya kupata kibali kutoka kwa mamlaka za kisheria  ili kupata uhakika wa chanzo cha kifo cha ndugu yao, aliyefariki Dunia Machi 25 na kuzikwa Machi 28.


Ndugu wamedai kuwa mara baada ya kutilia mashaka namna kifo cha ndugu yao kilivyotokea, ndiyo maana waliamua kufuatilia hatua zote lengo likiwa ni kuujua ukweli kama ndugu yao alifariki kifo cha kawaida ama aliuawa, kutokana na mazingira ya kifo hicho kuwa ni ya mashaka.

==>>Hapo chini ni taarifa ya Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hilo 


Mnamo tarehe 25.03.2020 majira ya saa 07:00 Asubuhi huko Chimala, Wilaya ya Mbarali na Mkoa wa Mbeya, TULIZO KONGA [34] Mkazi wa Chimala alifariki dunia nyumbani mnamo tarehe 27.03.2020 alizikwa katika makabuli ya Chimala na mazishi hayo yalihudhuriwa na ndugu wa pande zote mbili.

Kwa mujibu wa taarifa ya Daktari wa Hospitali ya Mission Chimala ilieleza kuwa marehemu alikuwa na tatizo la kiafya kwani alikuwa na uvimbe kichwani na walishampeleka Hospitali ya Mission Ikonda na baadae Hospitali ya Taifa Muhimbili na alitakiwa kufanyiwa upasuaji lakini ndugu wa marehemu walikataa kwa kuogopa angepoteza Maisha. Pia kutokana na tatizo hilo alikuwa amepata ugonjwa wa kifafa na hivyo tangu Madaktari waamue afanyiwe upasuaji marehemu hakuwahi kupata tiba ya upasuaji hadi mauti yanamkuta.

Baada ya wiki mbili kupita walifika Kituo cha Polisi Chimala kutoa malalamiko yako kwamba ;

1. Hawakujulishwa marehemu pindi anaugua 
2. Marehemu alipofikishwa Hospitali ya Mission Chimala hawakupata fursa ya kumuona mpaka walipoambiwa na Daktari kuwa amefariki 
3. Wakati wa kuchukua mwili wa marehemu kutoka Chumba cha kuhifadhiwa maiti Hospitali ya Meta hawakushirikishwa kumuandaa wala hawakumuona 

4. Wakati wa mazishi hapakuwa na ratiba ya kuaga mwili hivyo hawakumuona na wala hawakuwa na uhakika kama aliyezikwa ndiyo marehemu ndugu yao. Hivyo kwa ujumla walikuwa na mashaka na kifo cha ndugu yao.

Polisi tulifanya uchunguzi wa awali na hatimaye tuliwasiliana na Mkuu wa Mashtaka Mkoa kwa ajili ya kupata Amri ya Mahakama ya kufukua mwili. Baada ya amri ya Mahakama kutolewa, tulimuandaa Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Vifo [PATHOLOGIST] Dkt.Muller wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Mnamo tarehe 30.06.2020 majira ya saa 16:00 jioni huko katika makabuli yaliyopo Kijiji cha Igumbilo lilifanyika zoezi la kufukua mwili wa marehemu kwa kushirikiana na ndugu wa marehemu, uongozi wa serikali ya Kijiji, Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Vifo Dkt Muller na Jeshi la Polisi.

Baada ya kufukua mwili huo, ndugu wa marehemu walipata fursa ya kuuona na kuutambua na baadae uchunguzi wa kina ulienda kufanyika Hospitali ya Mission Chimala akiwemo Daktari kutoka upande wa ndugu wa marehemu. Pia katika uchunguzi huo kuna sampuli zilizochukuliwa na kupelekwa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Nyanda za Juu kwa uchunguzi zaidi.

Kwa sasa tunasubiri majibu ya kitaalamu kutoka kwa Daktari Bingwa aliyefanya uchunguzi huo na majibu kutoka Maabara ya Mkemi Mkuu wa Serikali kutokana na sampuli zilizopelekwa.

WITO WA KAMANDA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anatoa wito kwa ndugu wa marehemu na jamii kwa ujumla kuwa watulivu wakati tunasubiri majibu ya kitaalamu kutoka kwa Daktari Bingwa aliyefanya uchunguzi huo na majibu kutoka Maabara ya Mkemi Mkuu wa Serikali ili haki iweze kutendeka.


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527