SERIKALI KUJENGA KITUO KIKUBWA CHA UKUZAJI VIUMBE MAJI CHATO


Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Charles Kabeho akizungumza na ujumbe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi ya ujenzi ya Corporation sol uliofika ofisini kwake muda mfupi kabla ya kuelekea kijiji cha Rubambangwe ambako kitajengwa kituo kikubwa cha kukuzia viumbe Maji.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dokta Rashid Tamatamah (Kulia) akionesha mipaka ya eneo kinapotarajiwa kujengwa kituo cha kukuzia viumbe hai katika kijiji cha Rubambangwe wilayani Chato muda mfupi kabla ya kukabidhi eneo hilo kwa mkandarasi (Corporation Sol) ili aweze kuanza ujenzi wa kituo hicho.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dokta Rashid Tamatamah (kulia) akikabidhi mkataba na michoro ya majengo ya kituo cha kukuzia viumbe maji kwa Meneja wa Kampuni ya Corporation Sol Bw. Simeo Machibya Wilayani Chato (Geita).


Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia sekta ya Uvuvi imeikabidhi kampuni ya ukandarasi ya Serikali ya Corporation Sol eneo naf mkataba wa Ujenzi wa Kituo kikubwa cha Ukuzaji wa Viumbe Maji ili kazi hiyo ianze mara moja.

Makabidhiano hayo yaliyofanyika leo (08.07.2020) katika kijiji cha Rubambangwe kilichopo Wilaya ya Chato mkoani Geita yalifanywa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dokta Rashid Tamatamah ambaye mbali na kubainisha kuwa mradi huo utakuwa ni mkubwa kuliko yote hapa nchini, pia alielezea maeneo kadhaa yatakayohusiana na mradi huo.

Dokta Tamatamah alisema kuwa mradi huo utajumuisha ujenzi wa mabwawa yatakayokuwa na uwezo wa kutoa zaidi ya tani 10 kwa mwaka, jengo la vitotoleshi vya samaki ambalo litakuwa na uwezo wa kutoa vifaranga zaidi ya milioni mbili kwa mwaka, jengo dogo la kutengeneza chakula cha samaki na eneo la kuhifadhia samaki hao.

Aliongezea kuwa mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.8 mpaka kukamilika kwake na tayari Wizara ilishalipa fidia ya shilingi milioni 42 kwa wakazi waliokuwa wakifanya shughuli zao za kiuchumi katika maeneo hayo yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 28.

“Lakini pia hapa litajengwa darasa, bweni na ukumbi wa chakula kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wakuzaji viumbe maji wanaohitaji kujifunza au kuongeza ujuzi wa taaluma hiyo kwa kozi fupi za wiki mbili au tatu” Alisistiza Dokta Tamatamah.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe Maji ambao ndio wasimamizi wakuu wa kituo hicho pindi kitakapoanza kufanya kazi, Bw. Nazaeli Madala alisema kuwa kituof hicho kitakuwa ni ufumbuzi wa changamoto ya uchache wa samaki wanaopatikana kwenye vyanzo vya asili.

“Kituo hiki kitahudumia mikoa yote inayozunguka kanda ya ziwa na maeneo jirani na ukanda huo na tutawafundisha wafugaji wa samaki, maafisa ugani wa fani ya ufugaji wa samaki na pia kitatumika kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosoma katika ngazi mbalimbali huko vyuoni” Aliongeza Madala.

Madala alibainisha kuwa kituo hicho kitawasaidia kupata muongozo wa kujenga vituo vingine katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika, Nyasa na maeneo ya Pwani lengo likiwa ni kuhakikisha viwanda vyote vya samaki vilivyopo nchini havikosi malighafi.

Naye Afisa Mtendaji wa kijiji cha Rubambangwe Bi. Restituta Majura alisema kuwa mradi huo utawanufaisha sana wakazi wa kijiji hicho kwani mbali na kutoa ajira kwa wananchi watakaoshiriki kwenye hatua ya ujenzi, pia wanatarajia kunufaika na uwepo wa barabara itakayoelekea eneo la mradi kwani pia itawasaidia kufika kwenye zahanati ya kijiji inayoendelea kujengwa hivi sasa.

Kabla ya kuelekea kwenye eneo la ujenzi wa kituo hicho, Dokta Tamatamah akiwa na timu yake ya wataalam kutoka Wizarani walifika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Charles Kabeho ambaye aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kupeleka mradi huo kwenye Wilaya yake na kuahidi kufuatilia kwa ukaribu hatua zote za ujenzi wa kituo hicho hadi kitakapokamilika mnamo mwezi Oktoba mwaka huu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527