HILALI ALEXANDER RUHUNDWA AJITOSA UBUNGE JIMBO LA NGARA


Mwandishi wa habari wa Clouds Plus na msimuliaji mahiri wa simulizi bwana Hilali Alexander Ruhundwa amechukua fomu ya kuwania ubunge jimbo la Ngara mkoani Kagera kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ruhundwa ambaye amekuwa meneja wa vituo vya radio mbalimbali nchini na msimuliaji wa simulizi mbalimbali na mtangazaji wa Clouds Plus, amesema kwa muda mrefu ameguswa na jinsi Ngara isivyosonga mbele kimaendeleo licha ya kuwa mpakani mwa nchi za Burundi na Rwanda hivyo ameamua kuwania nafasi ya ubunge ili alete mabadiliko makubwa na kuifanya Ngara iwe kwenye ramani kimaendeleo. 

"Tangu nasoma shule ya msingi hadi nahitimu chuo kikuu, naona kero bado zipo palepale. Zamu hii Wanangara wakinipa ridhaa kupitia CCM nitawafuta machozi ya kiu ya maendeleo waliyoililia miaka mingi", Amesema Ruhundwa. 

Alipoulizwa vipaumbele vyake, Ruhundwa amesema kuwa atahakikisha Ngara inakuwa na viwanda vidogo vya kusindika mazao, kuhamasisha kilimo cha mazao ya biashara ambapo wakulima watakuwa na uhakika wa masoko, kuleta wawekezaji wa kuwekeza katika kilimo na viwanda.

Ameongeza kuwa anaamini katika teknolojia hivyo atahakikisha Ngara inakuwa na chui cha mafunzo ya TEHAMA ili kuandaa vijana waendane na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia. Pia atahakikisha anashirikiana na serikali na nchi jirani kufanikisha ujenzi wa chuo cha diplomasia Ngara chenye uwezo wa kudahili wanafunzi elfu kumi, kuondoa kero ya maji kwa wakazi wa Ngara kwa kujenga mradi mkubwa wa maji utakaohudumia takribani wakazi laki mbili.

Kuhusu sekta ya michezo, amesema kuwa atahakikisha anashirikiana na wataalam na serikali kufanikisha ujenzi wa uwanja wa mpira wa kisasa wilayani Ngara.

Upande wa miundombinu atahakikisha ujenzi wa barabara za Murugalama, Rulenge, Keza mpaka Nyakahula kwa kiwango cha lami, zingine zitakazojengwa kwa kiwango cha lami ni barabara za Rulenge, Bukiriro, Bugarama, Muganza hadi Murusagamba, barabara ya Rusumo hadi Lusahunga, barabara ya Nyamiaga hadi Rusumo pamoja na barabara ya Ngara, Mugoma hadi Mukikomero.

Ruhundwa mwenye kaulimbiu ya "Ngara Mpya, Ngara ya Wanangara", amesema kuwa endapo atapitishwa na chama chake CCM na hatimaye kuwa mbunge wa Ngara, atazingatia ushirikishwaji wa wataalam mbalimbali wazawa wa Ngara katika kila atakalolifanya ili kila mwanangara mwenye utaalam au ujuzi ashiriki kuijenga Ngara.

"Ngara ina wasomi wengi wenye taaluma mbalimbali ambao wakishirikishwa vema Ngara itabadilika kwa kiasi kikubwa" ameongeza Ruhundwa. 

Kuhusu vijana na akina mama na makundi mengine, amesema kuwa ataanzisha vikundi mbalimbali vya maendeleo na kuwawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu katika kutekeleza miradi mbalimbali. 

Vijana wasomi wasio na ajira atawawezesha kufungua kampuni mbalimbali kutokana na taaluma zao ambazo atahakikisha kuwa anawapatia kampuni kubwa za nje ya nchi washirikiane kibiashara. 

Licha ya kuwa na taaluma ya habari, Ruhundwa pia ni mjasiriamali mmiliki wa kampuni na ameshirikiana na wanafanyabiashara mbalimbali toka nchi za ulaya. 

Ni msomi wa shahada ya uandishi wa habari toka chuo kikuu cha Dar es Salaam, muumini wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu akiamini kuwa dunia inabadilika hivyo teknolojia haikwepeki.
Mwandishi wa habari wa Clouds Plus na msimuliaji mahiri wa simulizi bwana Hilali Alexander Ruhundwa akionesha fomu ya kuwania ubunge jimbo la Ngara mkoani Kagera kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527