MUME AMCHINJA MKE AKIMTUHUMU KUMNYIMA TENDO LA NDOA

Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake leo kuhusiana na mauaji ya mwanamke mmoja huko Majimoto Wilaya ya Mpimbwe mkoani humo. (Picha na George Mwigulu).


Na George Mwigulu, TimesMajira Online, Katavi
Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Dalali Malongo (20) Mkazi wa Kijiji cha Mipanga Kata ya Maji Moto Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi ameuawa kikatili kwa kuchinjwa shingo na mume wake aitwaye, Kisabo Joseph baaada ya mume wake kukasirishwa na kitendo cha mke wake kumnyima tendo la ndoa kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga tukio hilo la mauaji ya kikatili na ya kusikitisha lilitokea Julai 14, mwaka huu majira ya saa moja jioni huko katika Kijiji cha Mipanga Kata ya Maji Moto Wilaya ya Mlele.

Amesema,marehemu na mtuhumiwa walikuwa ni wanandoa waliokuwa wakiishi pamoja kama mume na mke,lakini katika ndoa yao inasemekana marehemu alikuwa akikataa kufanya tendo la ndoa pindi mume wake alipokuwa akihitaji kupatiwa tendo la ndoa na mke wake.

Hali ambayo inasadikiwa kuwa marehemu huenda alikuwa na mahusiano na mwanaume mwingine ambaye alikuwa akifanya nae tendo la ndoa na kumnyima mume wake tendo hilo.

Amesema, hali hiyo imemfanya mume wa marehemu achukie, hivyo siku ya tukio mume wa marehemu alimvizia marehemu wakati akienda kutaka maji kwenye chanzo cha Maji ya Moto.

Kamanda Kuzaga amesema, ndipo alipomvizia marehemu na kuchinja shingoni kwa kutumia kisu na kupelekea kifo cha marehemu huyo.

Baada ya kutekeleza mauaji hayo ya mke wake, Kisabo Joseph nae aliamua kujinyonga juu ya mti kwa kutumia kamba na kufariki dunia jirani na aliko mchinjia mke wake.

Kamanda Kuzaga aliwaambia wandishi wa habari kuwa,katika upelelezi wa awali wa tukio hilo Jeshi la Polisi limeweza kubaini kuwa chanjo cha mauwaji hayo yamesababishwa na wivu wa mapenzi.

Amesema, Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi hasa kwa wanandoa wawe na tabia ya kushughulikia masuala yao kifamilia kwa kuzingatia mwenendo mwema wa taratibu za kijamii kwa kushirikiana na viongozi wa dini na wa kimila katika maeneo yao ili kuepukana na matukio ya namna hiyo ndani ya jamii.
Chanzo - TimesMajira Online

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527