SALOME MAKAMBA ASHINDA KURA ZA MAONI KUGOMBEA UBUNGE SHINYANGA MJINI KUPITIA CHADEMA



Salome Makamba akizungumza mara baada ya kupata ushindi wa kura za maoni kugombea ubunge Jimbo la Shinyanga mjini kupitia CHADEMA.

Salome Makamba akiomba wajumbe kuvunja makundi na kuwa kitu kimoja ili kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu.



Na Marco Maduhu - Shinyanga
Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mwaka 2015, Salome Makamba, ameshinda kura za maoni za kupendekeza mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Shinyanga mjini kupitia Chama Cha Demokrasia Na Maendeleo (CHADEMA) ambapo majina yanapelekwa kwenye kamati kuu ya Chama kwa ajili ya kuteua mgombea wa uchaguzi huu 2020.

Zoezi la upigaji kura hizo limefayika leo Julai 15, 2020 kwenye ukumbi wa hoteli ya Ibanza, na kuhudhuriwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, ambapo walipiga kura za maoni za kumchangua mgombea ubunge wa jimbo la Shinyanga mjini, pamoja na Mbunge wa Viti maalum.


Aidha katika kura 177 zilizopigwa za Ubunge, Salome Makamba, amepata ushindi wa kura 75, akifuatiwa na Samsoni Ng'wagi kura 51, Emmanuel Ntobi kura 27, Paul Kaunda kura 10, Nicolaus Luhende kura nane, pamoja na Obed Jilala kura tano.

Kwa nafasi ya Ubunge wa Viti Maalum  kati ya kura 58 zilizopigwa, Salome Makamba alipata ushindi tena wa kura 24, ambapo wagombea wawili aliokuwa akishindana nao ambao ni Zena Gulam na Zainab Heri walifungana kwa kupata kura 17 kila mmoja.

Msimamizi wa uchaguzi huo Peter Shio ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Simiyu, amesema majina ya wagombea hao yatapelekwa kwenye kamati kuu ya CHADEMA, ambapo wao ndiyo watakuwa waamuzi wa mwisho wa kupitisha jina rasmi la mgombea ambaye atagombea Ubunge jimbo la Shinyanga Mjini.

Akizungumza mara baada ya kupata ushindi huo, Salome Makamba amewataka wana CHADEMA kuvunja makundi yaliyokuwapo wakati wa kampeni za kugombea kwenye kura hizo za maoni, na kuwataka kuwa kitu kimoja jambo ambalo litawapatia ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi huo mkuu wa Udiwani, Ubunge na Urais.

Awali wagombea wakisubiri matokeo ya kuchaguliwa kwenye kura za maoni kupeperusha bendera ya CHADEMA kugombea ubunge wa jimbo la Shinyanga Mjini.

Wajumbe wakiwa kwenye uchaguzi.



Wajumbe wakiwa kwenye uchaguzi.

Na Marco Maduhu- Shinyanga.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527