BINTI ATEKWA NA KUHIFADHIWA KICHAWI RUKWA

‘UKISTAAJABU ya Mussa Utaona ya Firauni’ ndivyo unavyoweza kusema kutokana na binti mwenye umri wa miaka 15 aliyepotea kwao wiki moja iliyopita katika mazingira ya kutatanisha, kupatikana akiwa ‘ametekwa na kuhifadhiwa kichawi’ nyumbani kwa Maria Birika (40) wilayani Kalambo mkoani Rukwa.

Mkasa huo unaelezwa kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa Kijiji cha Myunga kilichopo katika Kata ya Mkali katika Wilaya ya Kalambo, huku ukihusishwa na imani za kishirikiana.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Justine Masejo alithibtisha kutokea kwa mkasa huo, na kubainisha kuwa wananchi wenzake walimuua kikatili Birika kwa kuponda kichwani kwa vipande vya matofali wakimtuhumu kumteka na kumhifadhi kichawi binti huyo.

Alieleza kuwa binti huyo alipotea kwao wiki moja iliyopita, na baada ya msako mkali alipatikana akiwa amehifadhiwa nyumbani kwa mtuhumiwa.

“Baada ya taarifa ya kupotea kwa msichana huyo kuzagaa kijijini humo, juhudi za kumtafuta zilifanyika... hatimaye aligundulika akiwa amefichwa nyumbani kwa Maria Birika akiwa amelala fofo huku amefungwa kitambaa chekundu kichwani akiwa amepoteza uwezo wa kuzungumza,” alisema Kamanda Masejo.

“Maria alipohojiwa kuhusiana na mkasa huo, hakuwa na majibu,” alifafanua zaidi na kuongeza kuwa ndipo wanakijiji wenzake walipoamua kumfikisha katika ofisi za kata kwa hatua zaidi.

“Akiwa anahojiwa katika ofisi za kata, ghafla alitimua mbio akijaribu kutoroka, hapo ndipo watu wenye hasira walianza kumshambulia kwa kumponda kichwani na vipande vya matofali ya kujengea nyumba na kusababisha umauti wake...viongozi walijaribu kuwazuia lakini ilishindikana kwani walizidiwa nguvu,” alisisitiza.

Kamanda Masejo amekiri kuwa hakuna mtu yeyote aliyetiwa nguvuni kwa kuhusishwa na mkasa huo, huku juhudi za Jeshi la Polisi za kuwasaka watuhumiwa zinaendelea ili sheria ichukue mkondo wake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527