TAKUKURU MANYARA YAWAFIKISHA MAHAKAMANI WATENDAJI WAWILI KWA KUOMBA NA KUPOKEA RUSHWA


Na John Walter-Manyara
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa kushirikiana na jeshi la polisi wilayani humo, imemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro   Afisa Mtendaji wa kata ya Langai Anna John Mlomi kwa makosa ya kudai na kupokea rushwa ya  shilingi 100,000.

Taarifa iliyotolewa leo ijumaa  juni 19,2020 na mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara Holle Makungu imeeleza kuwa,  kosa hilo ni kinyume  na kifungu cha 15 cha sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Makungu amesema mwingine aliyeunganishwa katika mashtaka hayo ni afisa mtendaji wa kijiji cha Langai Masiar Sambana ambao walifikishwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa jeshi la polisi Magira Marwa na kufunguliwa kesi ya jinai namba CC 50 ya mwaka 2020.

Amesema baada ya kusomewa makosa yao mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Onesmo Nicodemo, watendaji wote wawili walikana kupokea rushwa hiyo.

Taarifa ya mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara imeeleza kuwa hadi wanaondoka mahakamani hapo ,washtakiwa walikuwa hawajatimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama.

Aidha uchunguzi wa TAKUKURU kuhusu shauri hilo umekamilika na kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Julai 1,2020.

Makungu  ametoa rai kwa watumishi wa Umma mkoani Manyara na Tanzania kwa ujumla, kwamba ili  kujiepusha na mkono wa sheria, wafanye rejea kwenye maandiko ya vitabu vitakatifu  ikiwemo Quran na Biblia  ambapo katika kitabu cha biblia Luka 3:12-14, watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali waliagizwa kutotoza kuliko walivyoamriwa na kwa watumishi wote wakatakiwa kutosheka na mishahara yao. Kwa wale  wanaokaidi yaliyoandikwa katika vitabu vitakatifu wafahamu kuwa mamlaka ziliwekwa na Mungu, hivyo wataendelea kupambana na mkono wa sheria.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post