SERIKALI YAZINDUA MWONGOZO WA TAIFA WAUENDESHAJI WA SHUGHULI ZA UTALII NCHINI TANZANIA WAKATI HUU WA JANGA LA CORONA


Serikali imezindua rasmi mwongozo wa uendeshaji wa Shughuli za Utalii nchini Tanzania wakati huu wa janga la Corona na kuwataka wadau sekta hiyo kuzingatia matakwa yaliyo katika mwongozo huo ili kulinda usalama wa Watanzania na watalii wanaowasili nchini kutembelea vivutio vilivyopo.

Akizindua mwongozo huo jana  jijini Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amewataka wadau wote wa Sekta watimize wajibu wao kwa kuhakikisha wageni wote wanaoingia nchini wanakuwa salama na wanaondoka salama pasipo kuambukizwa au kuambukiza wengine virusi vya Corona.

Dkt. Kigwangalla amesema Serikali imeamua kuzindua rasmi mwongozo huo ili kuilinda Sekta ya Utalii pamoja na afya za wadau wote wanaohusika na sekta hiyo na kuongeza kuwa hatua hiyo itaongeza na kujenga imani ya wageni wanaoitembelea Tanzania kutokana na masharti ya kiafya yaliyoainishwa katika mwongozo huo ambayo watoa huduma za utalii wanatakiwa kuyazingatia.

Ameongeza kuwa mwongozo huo huo utaisaidia biashara  ya Utalii kuanza upya wakati huu wa janga la CORONA ambapo Tanzania imeamua kufuangua  mipaka yake kufuatia baadhi ya nchi zikiwemo za Ulaya kuanza kufungua anga kwa  kuruhusu  mashirika makubwa ya ndege kuanzisha safari za ndege za abiria kutua  katika nchi hizo kuanzia mwezi Juni mwaka huu.

 Amebainisha kuwa Tanzania imeondoa masharti mengi ambayo yalikuwa yakikwamisha watalii wengi kuja nchini Tanzania likiwemo lile la mtalii kukaa Karantini kwa muda wa siku 14.

Dkt. Kigwangalla amewahakikishia wageni mbalimbali wanaopanga safari zao kuja nchini Tanzania waje bila hofu yoyote kwa kuwa Tanzania ni nchi salama.

MWISHO.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527