PIERRE NKURUNZIZA KUZIKWA LEO IJUMAA


 Rais wa zamani wa Burundi Pierre Nkurunziza aliyefariki ghafla tarehe 8 mwezi huu katika hospitali ya mkoa wa Karusi, anazikwa leo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Gitega.

Wananchi wa Burundi pamoja na wageni waalikwa kutoka ndani na nje ya nchi hiyo wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo.

Kiongozi huyo wa zamani wa Burundi, aliyeongoza taifa hilo kwa miaka 15, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 55.

Kifo chake kilikuja muda mfupi baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu na alikuwa akabidhi madaraka mwezi Agosti, lakini ripoti nchini humo zinasema alipata mshtuko wa moyo na kupoteza maisha.

Kulingana na taarifa ya serikali ya Burundi, hafla itaanzia kwenye 'hospital du Cenquantenaire Twese Turashoboye' iliyoko kwenye mkoa wa Karusi, mkoa jirani na Gitega, ambako maiti yake imehifadhiwa.

Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, yamekuwa yakiomboleza na wananchi wa Burundi kwa kupeperusha nusu mlingoti bendera za nchi zao na ile ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527