Breaking : RAIS WA BURUNDI PIERRE NKURUNZIZA AFARIKI DUNIA



Rais wa Burundi aliyemaliza muda wake Pierre Nkurunziza (55) amefariki dunia leo Jumanne Juni 9,2020.

Kulingana na msemaji wa serikali, Balozi Willy Nyamitwe, Rais Pierre Nkurunziza amefariki kwa mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 55 kinyume na uvumi unaoenezwa.

Serikali ya Burundi imetangaza siku saba za maombolezo na ametuma salamu za rambirambi kwa familia.

Aidha, serikali inasema kuwa alilazwa hospitalini Jumamosi iliyopita na akapata mshtuko wa moyo mapema hii leo.

Rais Pierre Nkurunziza aliyezaliwa Desemba 18, 1963 alikuwa ameratibiwa kumkabithi mrithi wake madaraka jenerali Evariste Ndayishimiye.

Ni mwanasiasa wa Burundi ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2005.

Alikuwa mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD, hadi alipochaguliwa kama rais wa Burundi.

2015, Nkurunziza alichaguliwa katika uchaguzi uliokuwa na utata na chama chake kwa muhula wa tatu ofisini.

Wafuasi wake na wanaompinga Nkurunziza walikosa kukubaliana katika suala la ikiwa ilikuwa halali kwake kugombea tena na maandamano yakafuata.Rais Nkurunziza akiidhinisha marekebisho ya katiba

Zaidi ya miezi miwili kulitokea maandamano ya kumpinga Nkurunziza ambayo yaliandamana na ghasia na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 100.

Mei 13, 2015, jaribio la mapinduzi dhidi ya Nkurunziza lilitokea akiwa nje ya nchi hiyo.

Mkuu wa mapinduzi hayo jenerali Godefroid Niyombare alidai kwamba amemng'oa mamlakani Nkurunziza lakini wanajeshi watiifu kwa Nkurunziza walikanusha madai hayo.

Nkurunziza ameongoza taifa hilo kwa miaka 15.

 Chanzo - BBC Swahili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527