DC KATAMBI AMSIMAMISHA KAZI AFISA MIPANGO MIJI JIJI LA DODOMA KWA KUDHULUMU ARDHI YA MJANE

Na Faustine Gimu,Dodoma

KUU wa wilaya ya Dodoma mjini Patrobasi Katambi ametangaza kumsimamisha kazi,Hadson Magomba,ambaye yupo kitengo cha mipango miji katika jiji la Dodoma kwa kushindwa kutenda haki kwa wananchi.

Katambi ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko yaliyotolewa na Mdala Mazengo wakati wa mkutano wa hadhara uliohusu kupokea malalamiko juu ya kudhurumiwa ardhi katika kata ya Ipagala Jijini  Dodoma   huku akitoa  agizo la  siku saba kwa mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwini Kunambi kuunda tume huru maalum  ya uchunguzi dhidi ya dhuruma ambayo amefanyiwa Mdala Anna Mazengo kwa kudhurumiwa viwanja vyake na kupewa mtu mwingine.

Katika mkutano huo Mdala Anna ambaye ni mjane toka mwaka 1985 na mwenye watoto kumi huku watoto wawili wakiwa walishafariki dunia amesema kuwa aliporwa maeneo yake katika maeneo ya swaswa extation  yenye ukubwa wa ekari sita.

Mdala Anna amesema kuwa pamoja na kuwa na eneo kubwa lakini afisa kitengo cha mipango miji wa Jiji la Dodoma ambaye alimtaja kwa jina la Hadson Magomba,alimnyanyasa kwa kutompa eneo lake huku akishindwa kumpa haki yake na kubadilisha matumizi na eneo hilo kuwapatia watu wengine.

"Mimi ni mjane tangu mwaka 1985 na mwenzangu aliniachia watoto kumi japo watoto wawili wameisha tangulia mbele ya haki,watoto waliobaki ninawatunza na nilikuwa na maeneo mbalimbali hasa maeneo ya swaswa zaidi ya heka sita.

" Cha kushangaza baadaye maeneo yangu yalitwaliwa na wakati yanatwaliwa nilikuwa na vielelezo vyote na nilijaribu kufuatilia lakini niliambulia vitisho na maneno ya kejeri na matusi.

"Nilienda katika kitengo cha mipango miji ili kuweza kusikilizwa lakini matokeo yake niliambulia kurushiwa barua na kama mbwa na Hadson Magomba jambo ambalo nilishindwa kupata msaada" alisema Mdala Anna.

Aidha Mdala Anna alisema kuwa kinachomshangaza ni kuona maeneo yake ualiyotwaliwa bila fidia anaona nyumba zikijengwa jambo ambalo alidhani labda ni nyumba za walimu jambo ambalo si kweli kumbe ni nyumba za watu binafsi.

Kutokana na malalamiko hayo Katambi ametoa agizo la kumsimamisha kazi Afisa wa kitengo cha mipango miji ya Jiji la Dodoma Hadson Magomba,huku akimwagiza mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi kuunda tume uchunguzi dhidi ya ofisa Huyo  ndani ya siku saba.

Katambi alisema kuwa tume hiyo inatakiwa kuundwa na watumishi kutoka ofisi ya mkuu wa Wilaya,Ofisi ya TAKUKURU,Kamati ya ulinzi na usalana pamoja na ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post