MKUU WA MKOA WA MARA ADAM MALIMA AIPONGEZA HALMASHAURI YA BUNDA KWA HATI SAFI

Na Immaculate Makilika- MAELEZO

Mkuu wa Mkoa wa Mara ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kupata hati safi kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.

Akizungumza hivi karibuni wakati  wa uwasilishaji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti  Mkuu wa  Hesabu za Selikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019, Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima  aliipongeza  Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kupata  hati safi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka wa fedha  2016/2017, 2017/2018 na 2018/2019.

“Halmashauri hii ni ya mfano katika mkoa wa Mara na ninawaomba msibweteke kwa vile mmepata mafanikio haya, bali muongeze bidii” alisema mkuu wa mkoa Malima

Aidha, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali katika  mkoa wa Mara, Patrick Lugisi alisema kuwa mafanikio hayo ni matokeo mazuri ya kazi wanayofanya watumishi wa Halmashauri ya mji wa Bunda.

“Ushirikiano na uwajibikaji  wa Menejimenti  ndio umepelekea Halmashauri hii  kuwa na hoja chache na kuwa na ufanisi, niziombe Halmashauri zingine kuiga mfano huu” alisema Lugisi.

Halmashauri ya mji wa Bunda ilianzishwa Mwaka 2015 na ilianza kutekeleza majukumu  yake Mwaka 2016. Hati safi kwa halmashauri hii imekuwa chachu ya kuongeza tija kwa watendaji wote na hivyo kuwawezesha wananchi kunufaika na huduma bora zinazotolewa  katika sekta za afya, elimu, maji,miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527