DC MBONEKO AONGOZA WADAU WA MAZINGIRA KUADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (kushoto) akimkabidhi miche ya miti Afisa Mazingira wa Manispaa ya Shinyanga, Ezra Manjerenga ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Kampeni ya Upandaji miti iliyopewa jina la Mtu na Mti, Mtu na Mti  Kwa Lugha ya Kisukuma "Mnhu na Nte, Nte na Mnhu!  
 ****
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko ameongoza Wadau wa Mazingira wakiwemo Askari wa JWTZ Shinyanga,Jeshi la Akiba na wananchi kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kufanya usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga.

Akizungumza leo Ijumaa Juni 5,2020 wakati wa Kilele hicho cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Mboneko amewataka wananchi kuendelea kupanda miti mbalimbali ikiwemo ya matunda katika maeneo yao ili kuhifadhi mazingira huku akisisitiza kuwa ni jukumu la kila mwananchi kupanda miti,kuilinda na kuitunza.

Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Manispaa ya Shinyanga, Ezra Manjerenga amesema licha ya kufikiwa kwa hatua kubwa za mafanikio katika utunzaji mazingira lakini bado changamoto ya uhifadhi wa mazingira ni kikwazo kinachosababishwa na shughuli za kibinadamu  hivyo ipo haja ya kila mtu kuhakikisha anatunza mazingira na kuepuka uchafuzi wa mazingira.


Amesema Shinyanga inapokea mvua wastani wa milimita 600 tu kwa mwaka na kufuatiwa na kipindi kirefu cha kiangazi kutokana na kukata sana miti kwa kipindi kifupi.

"Kati ya miti 100 inayopandwa bila uangalizi Ni miti 16 tu inayoweza kukua bila uangalizi, mingine hufa kwa sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mvua, mchwa, mizizi kukutana na mwamba (hard pan), shughuli za binadamu na magonjwa ya mimea. Hivyo uwezo wa miti kukua kwa njia asilia una changamoto nyingi",amesema Manjerenga.

"Ufugaji maeneo ya Mji umepelekea pale tunapootesha miti kuwa sehemu ya malisho ya mifugo kama mbuzi, n'gombe, punda na nk. Mfano, ni kawaida wazawa kuachilia mifugo usiku ili kutafuta malisho. Mbaya zaidi mbuzi hula vikonyo vya matawi na mti kudumaa",ameongeza Manjerenga.

"Ardhi ya Shinyanga haihifadhi maji ya kutosha kutokana na kutokuwa na miti ya kutosha. Uvukizaji (Evaporation rate) ni kubwa Shinyanga! hasa wakati wa kiangazi, hii ni nzuri lakini mvua hainyeshi Shinyanga kwa sababu hakuna miti ya kutosha kuhimili upepo usihamishe mawingu, matokeo yake wingu huhamia kwingine", amesema.

Manjerenga amesema Manispaa ya Shinyanga inatekeleza Kampeni ya Upandaji Miti inayojulikana kwa jina la Mtu na Mti, Mtu na Mti  Kwa Lugha ya Kisukuma Mnhu na Nte, Nte na Mnhu!  


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Ijumaa Juni 5,2020 Mjini Shinyanga.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akiwahamasisha wananchi kuendelea kupanda miti na kuitunza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Ijumaa Juni 5,2020 Mjini Shinyanga.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post