MNEC GASPER KILEO AMPONGEZA RAIS MAGUFULI ANAVYOPAMBANA NA CORONAMkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga, Gasper Kileo akiipongeza serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli namna ilivyopambana na ugonjwa wa COVID – 19. 

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi -CCM Taifa (NEC) Gasper Kileo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na hatua anazochukua katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Corona.

Kileo ametoa pongezi hizo leo Alhamis Juni 4,2020 wakati akikabidhi msaada wa kifaa cha kisasa cha kunawia mikono bila kugusa koki na vifaa vya kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya Corona vyenye thamani vya shilingi Milioni 8 kupitia Kampuni yake ya Uzalishaji Vinywaji Vikali ya East African Spirits (T) LTD Shinyanga katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Kileo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni  hiyo ya Uzalishaji Vinywaji Vikali ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga inayotengeneza vinywaji vya Diamond Rock na Hanson's Choice amesema vifaa hivyo vitatumika katika kuiongezea nguvu serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona huku akimpongeza Rais Magufuli jinsi alivyopambana na ugonjwa wa Corona.

“Ninaishukuru sana serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Amiri Jeshi wetu Mkuu, Rais wetu Mpendwa, Dkt. John Pombe Magufuli namna ilivyopambana na ugonjwa wa COVID – 19. Tumepambana na COVID-19 tofauti na nchi zote duniani na sasa wote ni mashahidi kwenye vyombo mbalimbali vya habari na Mitandao ya Kijamii kwamba dunia sasa inaangalia Tanzania imefanya nini kuiondoa Corona. wenzetu ndiyo wanafuta kile tunachofanya Tanzania”,amesema Kileo.

“Nimpongeze pia Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack kwa namna mnavyopambana dhidi ya Corona. Lakini pia niwapongeze Madaktari wetu wote nchi nzima mmepambana kwa kushirikiana na serikali na Mungu ametusaidia tumeweza. Naomba tuendelee kupambana mpaka pale Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli atakaposema silaha zetu tuziweke chini”,ameongeza Kileo.

Mkurugenzi huyo pia amewashauri wananchi kuendelea kunawa mikono na kwamba zoezi hilo liwe endelevu hata siku watakapotangaziwa kuwa Corona imefutika nchini Tanzania.

Vifaa vilivyotolewa na Kampuni hiyo ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga ni pamoja na kifaa cha kisasa cha kunawia mikono bila kugusa koki chenye thamani ya shilingi Milioni 6.8 kikiwa na masinki matano na tenki la maji lenye ujazo wa lita 1000 na vifaa vingine vya kujikinga na COVID-19 ikiwemo Vitakasa mikono,barakoa,gloves, pamba, sabuni za maji, cord clamp na pulse Oximeter vyenye thamani ya shilingi milioni 1.2.

Akipokea vifaa hivyo, Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ameishukuru Kampuni ya East African Spirits (T) LTD Shinyanga kwa mchango huo kwa ajili ya kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika mapambano dhidi ya Corona.

“Kimsingi mimi nimepokea vifaa hivi kwa niaba ya wananchi lakini hawa wananchi wanaonawa hapa wataendelea kukuombea kwa Mungu. Umetengeneza kitu kikubwa sana na pengine ndiyo maana walikuchagua kuwa MNEC wao hata wale wasiokuwa wa CCM sasa wanaona jinsi viongozi wa CCM na serikali ya CCM inavyojali wananchi. Huu ni mfano wa kutosha,niombe na viongozi wengine waige mfano wako”,amesema Mkuu huyo wa mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (katikati) akikata utepe wakati akipokea kifaa cha kisasa cha kunawia mikono bila kugusa koki na vifaa vya kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya Corona kutoka Kampuni ya Uzalishaji Vinywaji Vikali ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Muonekano wa Masinki ya kunawia mikono bila kugusa koki ambayo ni sehemu ya kifaa cha kisasa cha kunawia mikono kilichotolewa na Kampuni ya Uzalishaji Vinywaji Vikali ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga inayotengeneza vinywaji vya Diamond Rock na Hansons Choice kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Corona katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga, Gasper Kileo akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (aliyevaa kilemba cha bluu) namna ya kunawa mikono kwa kutumia kifaa cha kisasa cha kunawia mikono.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akinawa mikono kwa kifaa cha kisasa cha kunawia mikono bila kugusa koki kilichotolewa na Kampuni ya Uzalishaji Vinywaji Vikali ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Muonekano wa sehemu palipowekwa kifaa cha kisasa cha kunawia mikono iliyotolewa na Kampuni ya Uzalishaji Vinywaji Vikali ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Muonekano wa sehemu ya vifaa kwa ajili ya kujikinga na COVID-19 ikiwemo Vitakasa mikono,barakoa,gloves, pamba,cord clamp na pulse Oximeter vyenye thamani ya shilingi milioni 1.2 vilivyotolewa na Kampuni ya Uzalishaji Vinywaji Vikali ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (wa tatu kulia) akiishukuru Kampuni ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga kwa mchango wa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya East African Spirits (T) Limited Shinyanga, Gasper Kileo akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack sabuni ya kunawia mikono ili kukabiliana na COVID - 19 katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post