MGODI WA BARRICK BULYANHULU WATOA ZAWADI YA NG’OMBE, FEDHA KWA WANAFUNZI WALIMU NA SHULE ZILIZOFAULISHA KIDATO CHA NNE NYANG’HWALE

Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Bulyanhulu unaomilikiwa na Kampuni ya Twiga Minerals Corporation hapa nchini, umekabidhi zawadi zenye thamani ya shilingi milioni Tisa na elfu Hamsini kwa Wanafunzi, Wazazi, Walimu na Shule zilizofaulisha wanafunzi kwenye mtihani wa Kidato cha Nne Wiyalani Nyang’hwale.

Zawadi hizo zimekabidhiwa Jumamosi 27 Juni 2020 na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Fabian Yinza wakati wa hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Msalala wilayani Nyang’hwale mkoani Geita ya kuhitimisha mwaka wa kwanza wa mradi wa kuboresha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne wilayani humo unaojulikana kama PIP (Performance Improvement Program).

Akikabidhi zawadi hizo Kaimu Mkuu wa Wilaya alibainisha kwamba mradi huo ulibuniwa mwaka jana 2019 na ulitekelezwa kwa awamu tatu kwenye shule zote 10 za Sekondari wilayani humo kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Halmashauri, Mgodi wa Barrick Bulyanhulu na wadau mbalimbali.

“Wanafunzi 200 walishiriki kwenye mradi huu na kufanya mtihani wa taifa mwaka jana 2019, na kwa mara kwanza wilaya imefanikiwa kupata wanafunzi 20 wenye daraja la kwanza akiwemo msichana mmoja mwenye daraja la kwanza kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa wilaya hii kwa hivyo tunawashukuru sana Barrick Bulyanhulu tumepata matokeo chanya” ,alisema Mhe. Fabian Yinza.

“Hongereni sana wanafunzi mliofaulu, wazazi, walimu pamoja na wadhamini Barrick Bulyanhulu kwa juhudi na ushirikiano mliounyesha hadi kufikiwa kwa mafanikio hayo, nawasihi sana zawadi mtakazopewa leo na Kampuni ya Barrick Bulyanhulu uwe ni motisha wa kusonga mbele, na kuhamasisha wengine kufanya vizuri zaidi kwenye suala la elimu ili tupate wataalam watakaofanya kazi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kujengwa na serikali na wadau hapa nchini na Wilayani Nyang’hwale kama vile hospitali, vituo vya afya, zahanati, shule na viwanda”,alisema.

Kaimu Meneja wa Maendeleo ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Bi. Zuwena Senkondo alitaja makundi saba ya zawadi za kutambua waliofaulu na waliofanikisha ufaulu huo ikiwa sehemu ya motisha kwenye mradi huo wa PIP kwa mara kwanza.

“Kundi la kwanza la zawadi ni la wanafunzi wavulana wanne waliofaulu daraja la kwanza kwa pointi 12 hadi 13 ambapo wawili wenye point 12 tunawazawadia shilingi laki tano kila mmoja, na watatu wenye point 13 wanawazawadia laki tatu kila mmoja, Kundi la pili ni la wanafunzi saba wasichana waliofaulu daraja la kwanza na la pili, ambapo mwenye daraja la kwanza amezawadiwa fedha taslimu shilingi laki tano, na wengine wenye daraja la pili shilingi laki mbili kila mmoja.

Kundi la tatu ni la wazazi watano ambao watoto wao walifaulu vizuri kwa kupata daraja la kwanza, ambapo kila mzazi amezawadiwa Ng’ombe jike mmoja mwenye thamani ya shilingi laki tano, Kundi la nne ni walimu waliofaulisha vizuri zaidi kwenye masomo yao kwa alama A, na B wanazawadiwa kiasi cha shilingi laki moja hadi laki moja na ishirini na tano elfu kila mmoja kulingana na walivyofaulisha. Kundi la tano ni walimu 14 ambao wamefaulisha alama A kwenye masomo yao ambapo masomo ya sanaa walimu wanazawadiwa shilingi elfu hamsini kwa kila alama A na masomo ya sayansi shilingi elfu sabini na tano kwa kila alama A.

Kundi la sita ni zawadi ya shule moja iliyofaulisha kwa kuzingatia uwiano wa jinsia ambayo ni Shule ya Sekondari ya Shabaka iliyozawadiwa kiasi cha shilingi laki tano. Na kundi la saba ni la shule zilizofaulisha wanafunzi wengi kwa daraja la kwanza hadi la tatu ambazo ni Sekondari ya Nyang’hwale iliyofaulisha jumla ya wanafunzi hamsini, Sekondari ya Bukwimba iliyofaulisha wanafunzi 46 na Sekondari ya Kafita iliyofaulisha wanafunzi 38.

Akizungumza katika hafla hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale David Rwazo, alisema muasisi wa Mradi wa PIP ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Hamim Gwiyama ambaye kwa sasa ni Marehemu.

 “Tutamuenzi kiongozi huyu aliyekuwa mzalendo na mpenda elimu, tutahakikisha kwamba tunatimiza malengo ya program hii ambayo ni kuongoza matokeo ya kidato cha nne kimkoa na kushika nafasi bora za kitaifa, kwa mwaka huu wa kwanza tulilenga kupata wanafunzi 100 wenye daraja la kwanza hata hivyo tumefanikiwa kupata wanafunzi ishirini na hii ni ishara kwamba inawezekana, hasa baada ya kuona kwamba pia tumefaulisha msichana wa kwanza kwenye wilaya hii kwa daraja la kwanza jambo ambalo limefungua ukurasa mpya katika halmashauri yetu ya Nyang’hwale”,alisema.

Akitoa taarifa ya Idara ya Elimu Sekondari ya mradi wa PIP katika Halmashauri ya Nyang’hwale Afisa Elimu Vielelezo na Takwimu Mwl Felician James, alisema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo, Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kupitia mpango wake wa uwekezaji kwenye jamii (CSR), ulinunua vitabu 900 vya mazoezi ya masomo yote vilivyogawiwa katika shule zote 10, ili kuhakikisha wanafunzi wote wa kidato cha nne wanakuwa na vitabu vya masomo yote ili kujiandaa vyema na mitihani yao.

“Awamu ya pili ya mradi ilihusisha kambi ya mwezi mmoja ya wanafunzi 200 wa kidato cha nne ndani ya wilaya hiyo iliyofanyika na kuwawezesha wanafunzi kushiriki masomo ya ziada yaliyofundishwa na walimu wabobezi wa masomo mbalimbali wilayani humo, na awamu ya tatu ilihusisha walimu kupambanua changamoto za kwenye masomo mbalimbali za wanafunzi na kuwapatia masomo ya ziada na mtihani wa kujipima”, Alisema Afisa Elimu Vielelezo na Takwimu Mwl Felician.

Wakizungumza baada ya kupatiwa zawadi wanafunzi, wazazi, walimu na wakuu wa shule waliushukuru uongozi wa wilaya na halmashauri kwa kushirikiana na Barrick kutambua mafanikio yaliyopatikana.

“Walimu wamejitolea sana kunisaidia ili niweze kufaulu mtihani kwa kutufundisha bila kukata tamaa hadi muda wao wa ziada nawashukuru wazazi pia kwa kunipa nafasi ya kusoma pia wafadhili wa Barrick waliotupa chakula tukawa tunasoma tukiwa tumeshiba vizuri, nitajitahidi nisome kwa bidii nitakapoingia kidato cha tano ili niendelee kupata elimu zaidi.” Alisema Zainab Majaliwa ambaye ni mwanafunzi wa kwanza wa kike kupata daraja la kwanza wilayani humo akitokea katika Shule ya Sekondari ya Msalala.

“Ninaomba uongozi wa Mgodi uje unitembelee Ngo’ombe niliyezawadiwa leo naenda kumtumza azae na kunisaida kumsomesha mwanangu hadi afikie malengo”, alisema Charles Katemi mzazi wa Simon Charles aliyepata daraja la kwanza.

“Kila Sekondari ilipangiwa kufaulisha wanafunzi 10 wa daraja la kwanza sisi Kafita tumefanikiwa kupata wanafunzi watano wenye daraja la kwanza, lakini pia Mwalimu wetu mmoja amengoza kwa kupata zawadi kwa kufaulisha wanafunzi 3 wenye alama A katika somo la Bailojia, hivyo tunaamini tutafanya vizuri zaidi mwaka huu” alisema Mwalimu Mkuu wa Kafita Mwl. Felista Kamati.

“Shule yetu ya Sekondari ya Nyang’hwale imeongoza kiwilaya kwa kuwa nawanafunzi 50 waliofaulu kati ya daraja la kwanza hadi la tatu, na mimi nimepata zawadi kwa kufaulisha alama nzuri kwenye somo la History, tunashukuru sana mwanzilishi wa wazo hili, wadhamini wa mradi huu na viongozi wetu kwenye halmashauri yetu.” Alisema Mwl Steven Gumba Ombogo.


Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Fabian Yinza akizungumza wakati wa hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Msalala wilayani Nyang’hwale mkoani Geita ya kuhitimisha mwaka wa kwanza wa mradi wa kuboresha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne wilayani humo unaojulikana kama PIP (Performance Improvement Program).

Kaimu Meneja wa Maendeleo ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Bi. Zuwena Senkondo akitaja makundi saba ya zawadi za kutambua waliofaulu na waliofanikisha ufaulu huo ikiwa sehemu ya motisha kwenye mradi huo wa PIP kwa mara kwanza.Zainab Majaliwa ambaye ni mwanafunzi wa kwanza wa kike kupata daraja la kwanza wilayani humo akitokea katika Shule ya Sekondari ya Msalala.

Mzazi wa Zainab Majaliwa akikabidhiwa zawadi ya Ng’ombe Jike baada ya mtoto wake kupata daraja la kwanza

Wazazi waliopata zawadi ya Ng’ombe jike kwenye picha ya pamoja na watoto wao na mgeni Rasmi Mhe. Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Fabian Yinza, Kaimu Meneja wa Maendeleo ya Jamii Bi Zuwena Senkondo na maafisa wa halmashauri na wilaya ya Nyang’hwale mara baada ya kukabidhiwa zawadi.Mwalimu Steven Gumba Ombogo wa Sekondari ya Nyang’hwale akipokea zawadi ya pesa Taslimu shilingi 150,000 kwa kufaulisha kwa alama A na B somo la Historia katika shule yake.

Mwalimu Mkuu Shule ya Sekondari ya Kafita Mwl. Felista Kamati akipokea zawadi kwa niaba ya walimu wa shule yake waliofaulisha kwenye masomo Hesabu, Biolojia, na Kemia.

Baadhi ya wazazi ya wakitia saini hati za kuthibitisha kupokea zawadi

Walimu waliopokea zawadi

Wakuu wa shule waliopokea zawadi kwa ajili ya shule zao
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post