ASKOFU MSONGANZILA: TUENDELEE KUMUOMBEA RAIS MAGUFULI

Na Anitha Jonas – WHUSM,Shirati

Watanzania tuendelea kumwombea Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli ili aendelee kukua na kuongezeka imani na busara.

Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma ametoa wito huo hivi karibuni katika ibada maalum ya kumshukuru Mungu  iliyofanyika katika Parokia ya Shirati kwa ajili ya kumshukuru mungu kwa kulisaidia taifa dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona tofauti na ilivyotabiriwa na mataifa ya nje na hii ni kufuatia maono Mheshimiwa Rais yaliyosaidia taifa kukabiliana na janga la maambukizi ya Virusi vya Corona.

“Kwanini tung’ang’ane kupata taarifa za idadi za  vifo, taarifa hizi hazisaidii sana bali  zinaongeza hofu tu na pia hata  taarifa za kweli zinapotolewa baadhi ya watu wanabeza kwa Musoma hii mpaka sasa tuna kifo kimoja tu cha mgonjwa wa Corona hakuna taarifa zinazofichwa Kanisa Katolikili lina mfumo wa kupata taarifa kuanzia ngazi ya familia na tunafuatilia”, alisema Askofu Msonganzila.

Pamoja na hayo askofu huyo alieleza kuwa anafahamu katika kumshukuru Mungu makundi mbalimbali ya imani tofauti yalifanya maombi yao na katika Wilaya ya Shirati
anafahamu kuwa wapo wazee wa kijadi katika eneo hilo nao walifanya tambiko.

Askofu huyo alisisitiza kuwa pamoja na idadi ya maambukizi kupungua lakini ni vyema wananchi wanaendelea kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya wa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuvaa barakoa na kuepuka msongamano.

Kwa upande wa Chifu wa Rorya Ngoje Ogati alisema kuwa tangu janga hilo la virusi vya Corona lilipotangazwa wazee wa eneo hilo kutoka koo mbalimbali walifanya tambiko la kuzuia ugonjwa huo usifike katika eneo lao na mpaka sasa hakuna mtu hata mmoja katika eneo hilo amepata virusi hivyo.

“Katika ibada yetu ya tambiko tuliyofanya hivi karibuni ni la kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona katika nchi yote kwa ujumla pamoja na kushukuru kwa eneo la Rorya kutokupata maambukizi kabisa “,alisema Chifu Ogati.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Dkt.Emmanuel Temu alishukuru uongozi wa Wilaya ya Rorya kwa kuruhusu makundi yote ya kiimani ikiwemo la wazee wa jadi kufanya ibada ya kushukuru na kuliombea taifa.

Naye mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Rorya kutoka Kijiji cha Buturi Bi. Hudo Odemba alisema katika eneo lao hawajawahi kupata maambukizi ya virusi vya Corona na anaamini kuwa matambiko yaliyofanywa na wazee wa eneo hilo yamesaidia kuwakinga pamoja na taadhari wanazochukua za kunawa mikono kwa maji tiririka kila mara.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post