ASKARI POLISI WA FFU AFARIKI DUNIA KWA KUGONGWA GARI SHINYANGA...UZEMBE WATAJWA


Marehemu Idiphonce Nyamburi

Na Damian Masyenene – Shinyanga Press Club Blog
Askari wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoa wa Shinyanga, Idiphonce Sadick Nyamburi (32) mwenye namba G4793 PC amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati akitembea barabarani.


Ajali hiyo imetokea jana Juni 10, 2020 saa 9:30 alasiri katika barabara ya Dami hoteli Mjini Shinyanga, ambapo marehemu Idiphonce akiwa anatembea barabarani na mwenzake Ngassa Mabula (27) waligongwa na gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 788 DFW mali ya Nobert Masanja lililokuwa likiendeshwa na Paul John (38) mkazi wa Buzuka mjini Shinyanga.

Akisimulia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ambaye ni Ofisa Operesheni wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi Audax Majaliwa amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe ambapo dereva huyo aliwagonga watembea kwa miguu wawili akiwemo askari huyo ambaye aliumia vibaya kichwani na kuvunjika mguu wa kulia na akafariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.

Majaliwa ambaye ni , alisema mhanga mwingine wa ajali hiyo aliyetambulika kwa jina la Ngassa Mabula (27) mkazi wa kata ya Ndala mjini Shinyanga alipata majeraha madogo na alitibiwa na kuruhusiwa.

"Ajali hii ilitokea Juni 10, 2020 saa 9:30 Alasiri eneo la Mjini Kati barabara ya Dami Hoteli, ambapo gari hilo likiendeshwa na Paul John liligonga watembea kwa miguu wawili akiwemo askari wetu namba G4793PC wa kikosi cha FFU mkoa wa shinyanga aliumia vibaya kichwani na kuvunjika mguu wa kulia na kusababisha kifo chake wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.

"Majeruhi Ngassa Mabula alipata majeraha madogo na alitibiwa na kuruhusiwa. Uchunguzi wa shauri hili bado unaendelea, lakini dereva na gari lililosababisha kifo hicho tayari viko mikononi mwa polisi na uchunguzi ukikamilika hatua za kisheria zitachukuliwa," amesema Majaliwa.

Kamishna Msaidizi wa Polisi, Majaliwa aliwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuwa makini na utunzaji wa funguo za magari pale wanapokuwa wanahifadhi, na waangalie nani anatumia gari na ana utaalamu wa kiasi gani na kama hana leseni inakuwa ni tatizo.

"Ukiangalia tukio hilo limetokea kwa uzembe na mzembe lazima achukuliwe hatua za kisheria," amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527