AGAPE YAWAKUMBUKA WATU WENYE ULEMAVU MAPAMBANO DHIDI YA CORONA SHINYANGA




Shirika la AGAPE ACP linalotetea haki za wanawake na watoto mkoani Shinyanga, limewataka wananchi mkoani humo kuwakinga watu wenye ulemavu  dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona , pale wanapokuwa wakihitaji msaada wa kuwashika mkono na kuwavusha kwenye vivuko vya barabara.

Hayo yamebainishwa leo Juni 3,2020, na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE ACP John Myola, wakati akikabidhi kifaa cha kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kwenye ofisi ya Chama Cha Watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga (SHIVYAWATA), pamoja na kuwapatia elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Myola amesema watu wenye ulemavu hasa wasioona wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya Corona,kwa  sababu mara nyingi huwa wanahitaji msaada wa watu kuwavusha barabara na ni lazima washikwe mikono, hivyo endapo mtu huyo hakunawa mikono ama kujipaka Vitakasa atakuwa katika hatari ya kuambukizwa.

“Natoa wito kwa wananchi mkoani Shinyanga na maeneo mengine hapa nchini, tuwalinde watu hawa wenye ulemavu hasa wasiiona, pale tunapokuwa tukiwapatia msaada mbalimbali ikiwamo kuwavusha barabarani, tuzingatie unawaji mikono ama kujipaka Sanitizer, ili kuwahakikishia usalama wao wasipate maambukizi ya virusi vya Corona,”amesema Myola.

“Sisi AGAPE tumeguswa na kundi hili maalum, na ndiyo maana tumeamua kuwapatia kifaa hiki cha kunawia mikono kwa sabuni na maji tiririka kwenye ofisi yao, pamoja na kuwapatia elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona ili waendelee kubaki salama,” ameongeza.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga (Shivyawata) Richard Mpongo, amepongeza Shirika hilo kwa kuwajali na kuwapatia kifaa hicho pamoja na elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, jambo ambalo limewafanya kufarijika na wataendelea kujilinda.

Aidha amewataka wananchi mkoani humo kutowanyanyapaa watu hao wenye ulemavu hasa katika kipindi hiki cha Janga la maambukizi ya virusi vya Corona, bali pale wanapokuwa wakihitaji msaada wao wahakikishe wananawa mikono au kujipaka vitakasa mikono (Sanitizer) ndipo wawashike mikono ili wote wabaki kuwa salama.



TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Mkurugenzi wa Shirika la Agape mkoani Shinyanga , akitoa elimu ya kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona kwa watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga (SHIVYAWATA).

Mkurugenzi wa Shirika la Agape ACP mkoani Shinyanga John Myola akitoa elimu wa watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga (Shivyawata) namna ya uvaaji wa barakoa na kuzivua ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Afisa mradi wa utu wa msichana kutoka Shirika la Agape Sophia Rwazo akitoa elimu ya kujikinga na virusi vya Corona kwa watu wenye ulemavu.

Mkurugenzi wa Shirika la Agape ACP mkoani Shinyanga John Myola, akitoa elimu namna ya kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu mkoani Shinyanga (Shivyawata) Richad Mpongo (kushoto), akinawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara baada ya kupewa mafunzo namna ya kutumia kifaa hicho ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Katibu wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu mkoani Shinyanga (Shivyawata) Uel Nyange, akinawa mikono kwa sabuni na maji tirika mara baada ya kupewa mafunzo namna ya kutumia kifaa hicho ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Mwenyekiti wa Chama Cha Watu Wenye Ualbino mkoani Shinyanga Yunisi Zabron Manumbu, akinawa mikono kwa sabuni na maji tiririka.

Zoezi la unawaji mikono kwa sabuni na maji tiririka likiendelea .

Zoezi la unawaji mikono  kwa sabuni na maji tiririka likiendelea.

Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga (Shivyawata) Richard Mpongo akiishukuru AGAPE kwa kuwapa elimu namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona , pamoja msaada wa kifaa cha kujikinga na Maambukizi ya virusi hivyo.

Na Marco Maduhu- Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527