Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa Kilimo Mhe.Japhet Hasunga amewasilisha bungeni jijini Dodoma Muswada wa Sheria ya Afya ya Mimea Na.2 wa Mwaka 2020.
Akiwasilisha Muswada huo leo Mei 19,2020 Waziri Hasunga amesema madhumuni ya muswada huo ni kutungwa kwa sheria ya Afya ya mimea ya mwaka 2020 na lengo la sheria hiyo ni kuunganisha sheria ya Hifadhi ya Mimea Sura 133 na sharia ya Taasisi ya utafiti wa viuatilifu vya kitropiki [TPRI] Sura ya 161 ili kuondoa upungufu katika mfumo wa sasa wa kisheria na mwingiliano wa sheria hizo zilizopendekezwa kufutwa.
Aidha,Waziri Hasunga amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha mfumo utakaosaidia kuondokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za uingizwaji na usambazaji wa viuatilifu bandia.
Waziri Hasunga ameendelea kufafanua kuwa Tanzania imeridhia itifaki na mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa inayosimamia afya ya mime na matumizi ya viuatilifu kwenye kilimo kwa lengo la kukidhi matakwa ya masoko.
Mikataba hiyo ni pamoja na mkataba wa kimataifa wa hifadhi ya mimea [International Plant Protection Convetion -IPPC] wa Mwaka 1997 ambapo Tanzania iliridhia Oktoba 21,2005.
Waziri Hasunga ametaja mambo muhimu katika Muswada wa sheria ya Afya ya mimea Na.2 wa Mwaka 2020 ni pamoja na kuanzisha mamlaka itakayosimamia afya ya mimea na viuatilifu pamoja na kuweka utaratibu wa kusimamia uingizwaji ,utengenezaji wa usambazaji na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu .
Akiwasilisha maoni na Ushauri wa kamati ya kudumu ya Bunge ya kilimo ,mifugo na maji kuhusu Muswada wa sheria ya Afya ya Mimea ,2020 ,Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Christine Gabriel Ishengoma amesema Kulingana na Vifungu 21, 22 na 23 vya Sheria pendekezwa, inabidi mtu anayetaka kuingiza mimea nchini kupata kibali kutoka kwa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu itakayoanzishwa huku Kanuni za Mbegu (Seeds Regulations, 2007) nazo zinaelekeza kuwa kibali cha kuingiza mbegu nchini (Kanuni ya . 33) au kusafirisha mbegu nje ya nchini (Kanuni ya 34) kitatolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Kilimo hivyo Kuna haja ya kuhakikisha kuwa hakuna mwiingiliano wa mamlaka katika utekelezaji wa Sheria inayopendekezwa na Sheria ya Mbegu (2003).
Akiwasilisha maoni ya kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,Msemaji mkuu kambi hiyo katika Wizara ya Kilimo Pascal Haonga ameishauri serikali kutilia mkazo Zaidi katika kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu kwani visipotimika ipasavyo vinaweza kuleta madhara kwa afya binadamu ikiwa ni pamoja na Kansa na upofu.
MWISHO.